Saturday, February 25, 2012

Kampeni ya maliza malaria yapamba moto Zanzibar

Na Is-haka Omar ZPC
Kitengo cha kupambana na malaria Zanzibar kimeanza kazi za usajili wa kaya ikiwa ni matayarisho ya ugawaji wa vyandarua unaotarajiwa kufanyika mapema mwezi ujao.
Kazi hizo zilizoanza jana zitaendelea kwa muda wa siku tatu ili kupata idadi sahihi ya kaya zitakazopatiwa vyandarua ambapo kwa mujibu wa kitengo hicho kiasi vyandarua laki saba vitagaiwa bure kwa wananchi wa Unguja na Pemba..
Meneja wa kitengo cha kupambana na malaria Bw.Abdalla Suleiman amesema kiasi ya vijana elfu mbili wa wilaya zote wamepatiwa mafunzo ya usajili wa kaya na kusambaza vyandarua kwa wananchi.
Amefahamisha hatua hiyo itasaidia kufanikisha ugawaji wa vyandarua na kutoa wito kwa wananchi kutodharau usajili huo ili kila kaya ipate chandarua kwa lengo la kutomeza malaria Zanzibar.

Balozi Seif afanya mazungumzo na Balozi wa EU Tanzania

Na Is-haka Omar ZPC
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amefanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Ulaya (E.U) nchini Tanzania Bw.Filiberto Ceriani.
Katika mazungumzo yao viongozi hao walielezea haja ya kuongeza ushirikiano kati ya pande hizo mbili na Bw.Filiberto amesema umoja wa ulaya umeandaa mpango wa kuzijengea uwezo jumuiya na taasisi za kiraia utakaogharimu karibu Euro milioni tatu.
Amesema mpango huo utaenda sambamba na utowaji wa mafunzo kwa watendaji wa sekta ya sheria ili kuwajengea mazingira bora ya uwajibikaji sekta hiyo.
Nae Balozi Seif amesema Zanzibar inaendelea kupiga hatua za maendeleo kufuatia uendeshaji wa mfumo wa serikali ya umoja wa kitaifa.
Hata hivyo Balozi Seif amesema bado yapo maeneo muhimu ya huduma za kijamii kama maji, elimu na afya hayajafikia kiwango kilicholengwa.
Hivyo amesema msaada zaidi unahitajika kutoka kwa taasisi na washirika wa maendeleo juhudi hizo za serikali za kuwaletea maendeleo wananchi.

Msumbiji yaitaka Tanzania kufukiria njia ya kurudisha vikao vya pamoja

Na Is-haka Omar ZPC
Msumbiji imeiomba Tanzania kufikiria uwamuzi wa kurejeshwa tena utaratibu wa kuwa na vikao vya pamoja kati ya pande hizo mbili ambao ulilenga zaidi kuimarisha ujirani mwema.
Ombi hilo limetolewa na Balozi wa Msumbiji nchini Tanzania Bw.Zakaria Kupella wakati alipofanya mazungumzo na makamu wa pili wa rais wa zanzibar balozi Seif Ali Iddi hapo ofisini kwake vuga mjini Zanzibar.
Amesema tanzania ilikuwa mstari wa mbele katika kusaidia ukombozi wa mataifa ya bara la afrika ikiwemo jirani yake Msumbiji hivyo ni vyema vikao vya ushirikiano vikafufuliwa kwa nia ya kulinda umoja na udugu wa sehemu hizi mbili.
Amesistiza kwamba yapo maeneo mengi ambayo wananchi wa pande hizo mbili wamekuwa wakishirikiana pamoja hasa ikizingatiwa kwamba nchi hizo zimepakana.
Balozi huyo amesema ni vyema ukaandaliwa utaratibu wa kuyaunganisha makundi ya vijana wa pande hizo mbili kujenga taifa katika mpango wa kujitolea.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema uhusiano wa pande hizo mbili unafaa uelekezwe zaidi katika uchumi badala ya siasa ambapo ameiomba msumbiji kufikira wazo la kutoa wataalamu kuja zanzibar katika kutoa elimu katika sekta ya uvuvi wa kamba.
Balozi Seif amesema dunia imeshuhudia kiwango kikubwa cha bidhaa ya kamba inayozalishwa msumbiji na kusafirishwa nje ya nchi na kuipatia kipato kikubwa nchi hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa mjini azuwiya ujenzi katika wilaya yake

Na Is-haka Omar ZPC
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Bw.Abadalla Mwinyi Khamis ametoa agizo la kuzia uuzaji wa viwanja na ujenzi wa aina yoyote katika eneo ambalo wananchi wa shehia ya mbuzini wanalihitaji kulitumia kwa ujenzi wa miradi ya kijamii.
Amesema tabia inayofanywa na baadhi ya watu kuuziana viwanja kiholela si utaratibu unaofaa hivyo ameuagiza uongozi wa wilaya ya Magharibi kushirikiana na wananchi wa eneo hilo kuliomba eneo hilo kwa wizara ya ardhi ili kupata umiliki na kulitumia kwa malengo yao.
Ametoa agizo hilo wakati wa ziara huko mbuzini kufuatia malalamiko ya wananchi kuhusu kuwepo kwa baadhi ya viongozi kuuza viwanja kwenye neo hilo.
Nao wananchi wa Mbuzini wameelezea kusikitishwa na vitendo vinavyofanywa na baadhi ya viongozi kuuza viwanja ovyo pamoja na kuutupia lawama uongozi wa jimbo kwa kushindwa kufuatilia suala hilo.
Wakati huo huo mkuu huyo wa mkoa amefanya ziara shehia ya Fuoni Pangawe kuona uharibifu wa mazingira unaofanywa kwa uchimbaji mchanga na kuutaka uongozi wa shehia hiyo kuimarisha polisi shirikishi jamii ili walinde maeneo yao.

Friday, February 24, 2012

Kiongoni watakiwa kuinua sanaa

Na Is-haka Omar ZPC
Katibu Mkuu Wizara ya Kazi,Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika Bi.Asha Ali Abdallah amekitaka kikundi cha sanaa cha skuli ya Kiongoni kuendeleza sanaa ya ngoma kwani vipaji vikiendelezwa hupelekea kuwa sehemu ya kujifunza na kupata ajira.
Hayo ameyaeleza wakati wa kukabidhi fedha taslimu sh.laki tano kwa kiongozi wa kikundi hicho cha sanaa huko ofisini kwake Mwanakwerekwe.
Amesema lengo la kutolewa kuwa fedha hizo ni kuendeleza kikundi hicho kiweze kukua kisanaa na kuinua vipaji vya wasanii.
Bi.Asha amefahamisha kuwa msaada huo umetolewa kufuatia ahadi alizotoa makamo wa pili wa rais Mhe.Balozi Seif Ali Idd katika uzinduzi wa soko la jumapili (sunday market) huko michenzani.
Nae mwalimu wa kikundi hicho Bw.Shaabani Naim Suleiman ametoa shukrani zake kwa makamo wa pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi kwa kutimiza ahadi yake pamoja na kuahaidi kuwaendeleza wasanii.
Kikundi hicho kima wanafunzi 15 na viongozi 3 na wanajishughulisha na ngoa za msewe,chaso na kurungu.
Pamoja na hayo kazi kubwa ya kikundi hicho ni kutoa elimu kwa jamii juu ya mambo mbalimbali kupitia sanaa ya ngoma ikiwemo utunzaji wa mazingira ,dawa za kulevya na ukimwi.

Waandishi watakiwa wawe wafuatailiaji wa kina juu ya matukio na masuala yawahusuo watu wenye kuishi na ulemavu

Na Is-haka Omar ZPC
Waandishi wa habari nchini wametakiwa kushiriki kikamilifu katika kufuatilia kwa kina na kuandika habari na matukio mbalimbali ya watu wenye ulemavu ili waweze kupata haki zao za msingi kisheria.
hayo yameelezwa na mwenyekiti wa bodi kutoka ofisi ya umoja wa watu wenye ulemavu Zanzibar Bw.Ali Omar Makame wakati akifungua mafunzo ya siku 3 huko katika ukumbi wa jumuiya hiyo weres kwa waandishi wa habari juu ya kutambua haki za msingi za watu wenye ulemavu kisheria.
Amesema waandishi wa habari watumie taaluma yao katika kuelimisha jamii kwa kuandika habari na kufichua maovu wanayofanyiwa watu wenye ulemavu ili nao wapate haki zao za msingi kama watu wengine katika jamii.
Aidha Bw.mMakame amefahamisha kuwa watu wenye ulemavu wanatakiwa kushirikishwa katika mambo mbalimbali yanayowahusu hususani kijamii,kiuchumi na kisiasa.
Nae mwezeshaji katika mafunzo hayo bw.ali saleh amesema watu wenye ulemavu katika mkataba wa kimataifa wanatakiwa kuwa na fursa iliyo sawa kwa manufaa ya taifa katika nyanja zote za kijamii na katika hali yoyote inayojumuisha upatikanaji wa elimu, habari, mawasiliano na mazingira ya kimaumbile.
Bw.Saleh amesema kuwa sheria namba 9 ya mwaka 2006 ya Zanzibar ya watu wenye ulemavu inamapungufu katika suala zima la utekerezwaji kwani walengwa wa sheria hiyo hawapatiwi haki zao kwa mujibu wa sheria inavyoeleza hususani katika ujenzi wa majengo ya serikali pamoja na asasi za kiraia hawazingatii miundo mbinu inayoendana na mazingira halisi ya watu wenye ulemavu na kusababisha usumbufu mkubwa bindi wanapotaka kupata huduma mbalimbali za kijamii.

Serikali yatakiwa kulipatia ufumbuzi tatizo la ubovu wa barabara ya Kinuni-Unguja

Na Is-haka Omar ZPC
Wananchi wa shehia ya Kinuni wameiomba serikali kuwatatulia tatizo la ubovu wa barabara ya eneo hilo ili kuwaepushia usumbufu wanaopata.
Wamesema wakati umefika kwa serikali na taasisi binafsi kuweka mikakati mbalimbali ili kuona barabara za maeneo mbalimbali ikiwemo ya eneo hilo zinajengwa na kuimarishwa kwa lengo la kuwaondolea wananchi usumbufu katika utekelezaji wa shughuli zao za kila siku.
Wakizungumza na waandishi wa habari hizi wamesema wamekuwa wakikabiliwa na usumbufu mkubwa pale wanapokuwa safarini kutokana na ubovu wa barabara hiyo jambo ambalo linawaresha nyuma maendeleo yao.
Hivyo wamesema kukosekana kwa barabara ya uhakiki katika shehia hiyo kunasababisha kutofanyika shughuli zao kwa ufanisi zaidi

ZAWA yatakiwa kulipatia ufumbuzi tatizo la maji Chumbuni

Na Is-haka Omar ZPC
Mamlaka ya maji zanzibar ZAWA imeombwa kulitafutia ufumbuzi tatizo la maji safi na salama linalowakabili kwa muda mrefu wananchi wa maeneo ya chumbuni.
Wakizungumza na waandishi wa habari hizi wananchi wa shehia hiyo wamesema tatizo hilo linarejesha nyuma shughuli zao za kujiletea maemdeleo na kuathiri maisha yao ya kila siku.
Wamesema maji wanayoyategemea hivi sasa ni ya kisima cha Chumbuni na Masjdi Raudha ambayo wanalazimika kulipia shilingi 50 kwa kila ndoo.
Hivyo wameitaka mamlaka hiyo kulishughulikia tatizo hilo kwa umakini kwa vile maji ni huduma muhimu katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za jamii

Miti elfu moja yatarajiwa kupandwa ikiwa ni miongoni za njia bora za kuhifadhi misitu Zanzibar

Na Is-haka Omar ZPC
Kiasi ya miti elfu moja inatarajiwa kupandwa katika sehemu za wazi za kijiji cha Jendele hadi Cheju ikiwa ni harakati za kuimarisha hifadhi ya misitu na utunzaji wa mazingira katika vijiji hivyo.
Mradi huo unatarajiwa kutekelezwa na kamati ya uhifadhi wa misitu ya asili ya cheju pembezoni mwa barabara ambapo hivi sasa wanasubiri utekelezaji wa ujenzi wa barabara inayounganisha vijiji hivyo uanze ili kuona maeneo muafaka yatakayotumika.
Sheha wa shehia ya cheju Bw.Kassim Suleiman Mdunga amesema wameshatoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa idara ya mistu ili kupatiwa msaada na maelekezo zaidi juu ya zoezi hilo.
Amefahamisha kuwa shehia hiyo imeamua kupanda miti ya miembe boribo ambayo ni miongoni mwa mimea inayoanza kupotea kutokana na ongezeko la watu kujihusisha na shughuli za ukataji miti kwa ajili ya kujiongezea kipato na matumizi ya kijamii.
Kwa upande wake sheha wa shehia ya jendele Bw.Ame Makame Rajab ameiomba serikali kuhamasisha jamii katika kutafuta mbinu mbadala zitakazosaidia kupumguza vitendo vya ukataji miti kiholela katika shehia hizo.

Oman yasaidia Zanzibar kimatibabu

Na Is-haka Omar ZPC
Serikali ya Oman imekusudia kutoa msaada wa matibabu nje ya nchi kwa watoto kuanzia mwaka mmoja hadi miaka kumi na sita wanaosumbuliwa na ugonjwa wa moyo.
Waziri wa afya Mhe.Juma Duni amesema kuwa wagonjwa hao watapelekwa katika hospitali ya Narayana nchini india kuanzia mwazoni mwa mwezi ujao kwa gharama zitakazotolewa na serikali ya oman ambapo mgonjwa mmoja anakisiwa kugharimu kiasi ya dola elfu nne hadi tano.
Akizungumza na waandishi wa habari amesema hatua hiyo itakuwa ya kuendela ikiwa ni juhudi ya wizara hiyo katika kutafuta ufadhili wa matibau ya watoto ambapo katika hatua ya awali watoto kumi hadi ishirini watasafirishwa kwa ajili ya matibau zaidi.
Mhe Duni amefahamisha kuwa timu ya madaktari watatu kutoka hospitali ya Narayana wanaendelea na zoezi la kuchunguza watoto hao kisiwani pemba na kwa unguja watoto 73 wamegundulika kuhitaji matibabu zaidi.
Hivyo ameishukuru serikali ya oman kwa ufadhili huo baada ya kuelewa tatizo hilo ikiwa ni juhudi za kusadia kuimarisha ustawi wa afya za watoto nchini.

Skuli ya Kisiwandui kufaidika na mtandao wa teknolojia

Na Is-haka Omar ZPC
Mbunge wa jimbo la kikwajuni Mh.Hamad Yussuf Masauni amekabidhi hundi ya shilingi milioni mbili kwa kampuni ya milenium enginearing ya Dar-es-salaam kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha teknohama ndani ya jimbo hilo.
Akikabidhi hundi hiyo amesema ujenzi huo utajengwa kwa awamu ambapo awamu ya kwanza itagharimu shilingi milioni tano ambacho kitawasaidia wananchi kitajengwa ndani ya eneo la skuli ya Kisiwandui kitawawezesha vijana kujiingiza katika mtandao wa sayansi na teknologia.
Akizungumzia suala la uimarishaji wa barabara za ndani ya jimbo hilo mh masauni amesema wamo mbioni kuzifanyia matengenezo ili kuziweka katika hali ya kuridhisha.
Nae mhandisi kutoka kampuni hiyo Bw Ali Bakari Ali amesema kampuni hiyo inashughulikia miradi mbali mbali ya maendeleo ya wananchi ambapo kwa hapa watajenga kituo hicho cha teknohama ili kuendeleza elimu nchini.
Aidha amewataka wananchi kufuata taratibu za kisheria wakati wanapotaka kujenga pamoja na kupata ushauri wa kitaalamu ili kuepusha usumbufu unaoweza kujitokeza .

Wednesday, February 22, 2012

JUMMAZA yakusudia kuziweka nyumba za maendeleo Kilimani kuwa safi

Na Is-haka Omar ZPC Zanzibar
Katibu wa jumuiya ya uhifadhi wa mazingira na maendeleo Zanzibar JUMMAZA Bw Ramadhan Fadhil amesema jumuiya hiyo imedhamiria kulifanya eneo la nyumba za maendeleo kilimani kuwa katika hali ya usafi na salama .
Akizungumza na waandishi wa wahabari wa vyombo mbalimbali huko kilimani amesema hatua hiyo imekuja kufuatia eneo hilo kuwa katika hali isiyoridhisha na kuhatarisha maisha ya wakaazi wa eneo hilo .
Bw Ramadhan amesema tayari jumuiya yake imeshaanza kazi ya kuondoa taka zilizomo pembezoni mwa nyumba hizo na kusafisha majani yaliyopo kweye eneo hilo .
Amesema baada ya hatua hiyo wanatarajia kusafisha mitaro na kuchukua taka nyumba hadi nyumba zoezi ambalo linatarajiwa kuwa la kudumu
Aidha ameiomba serikali na taasisi binafsi kuunga mkono jitihada za jumuiya hiyo iweze kufanikisha kazi ya kuweka mazingira safi na salama

ZAFEPED yatakiwa kubuni mbinu mbadala za kuwasaidia wananchi kutokana na umasikini

Na Is-haka Omar ZPC Zanzibar
Mkuu wa wilaya ya kusini Bw Haji Makungu Mgongo amewataka wanajumuiya ya kupambana na umasikini na uharibifu wa mazingira ZAFAPED kubuni mbinu mbali mbali zitakazowasaidia wananchi kuondokana na umasikini .
Akizungumza na viongozi wa jumuiya hiyo ofisini kwake amesema wananchi wengi wa wilaya ya kusini wanatengemea misitu katika kupata ajira hali inayosababisha uharibifu mkubwa wa mazingira .
Amesema ili wananchi waondokane na tatizo la uharibifu wa mazingira ipo haj ya kutoa elimu kuondokana na uharibifu wa mazingira ikiwemo misitu katika wilaya hiyo tatizo ambalo limedumu kwa muda mrefu .
Nae Mkurungezi wa jumuiya hiyo Bw. Faida Khamisi Ali amesema lengo kuu la jumuiya hiyo ni kuwapatia wananchi elimu na mbinu za kupambana na umasikini .
Jumuiya hiyo inafanya kazi zanzibar katika shehia za wilaya ya kusini ikiwemo mtende ,pete na kajegwa kwa kupitia mradi wa hima na Care tanzania ambapo mradi huo utakuwa wa mienzi sita .

Maalim Seif awataka watendaji wa chama cha CUF kuwa karibu na wanachama wao

Na Is-haka Omar ZPC Zanzibar
Katibu mkuu wa chama cha wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad amewataka watendaji wa chama hicho ngazi ya wilaya kufanya kazi kwa karibu na wanachama ikiwa ni hatua muhimu katika kukijenga chama chao.
Amesema watendaji hao wana nafasi kubwa katika kukijenga na kukiimarisha chama hicho, ikizingatiwa kuwa wao ndio wenye mawasilianao ya karibu zaidi na wanachama pamoja na wananchi kwa ujumla.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ametoa wito huo leo katika hoteli ya mazsons shangani mjini zanzibar, wakati akifungua semina elekezi kwa wenyeviti na makatibu wa wilaya wa chama cha CUF, yenye lengo la kujadili dhana ya utumishi wa umma.
Amewataka wajumbe wa mkutano huo kuijadili dhana hiyo kwa umakini mkubwa, kwa kuzingatia zaidi maslahi na maendeleo ya chama hicho, sambamba na kuhimiza suala la uwajibikaji kwa viongozi wa ngazi zote za chama.
Semina hiyo imehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa chama hicho wakiwemo wenyeviti na makatibu wa wilaya kutoka wilaya zote za unguja na Pemba.

Mkuu wa Wilaya awataka watendaji wa wilaya ya mkoani kushirirki ipasavyo katika kamapeni ya chanjo ya Surua

Na Is-haka Omar ZPC Zanzibar
Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Bw. Jabu khamis Mbwana amewataka watendaji wa Wilaya za Mkoani Pemba kushirikiana ipasavyo katika kukabiliana na ugonjwa wa surua .
Mkuu huyo wa wilaya ya mkoani amesema viongozi wa afya ,masheha wa shehia nane za wilaya hiyo, madiwani na viongozi wa vyama wanapaswa kushirikiana pamoja katika kulikabili tatizo la ugonjwa wa surua katika shehia hizo.
Ndugu Mbwana ametoa wito huo huko ukumbi wa Umoja ni Nguvu wakati akizungumza na viongozi na walimu wakuu wa skuli saba za shehia hizo ambazo zinakabiliwa na mripuko wa maradhi ya surua katika shehiya hizo.Shehia za Mizingani,Mgagadu,Ngwachani,KisiwaPanza,Chokocho,stahabu,wambaa, na shumbageni zinaelezwa kukumbwa na mripuko mkubwa ugonjwa wa surua katika kisiwa cha Pemba. Ndugu Mbwana amefahamisha kuwa jambo lililopelekea kutokea kwa mripuko wa maradhi hayo ni wananchi wakati wa chanjo iliyopita kudharau kuwapeleka watoto kupatiwa chanjo licha ya elimu kutolewa kabla ya chanjo hiyo.
Pamoja na hayo amesema kutokana na tatizo hilo wizara ya afya kwa kushirikiana na serikali ya wilaya ya mkoani inakusudia kutoa chanjo hiyo.

NEC maandalizi ya uchaguzi mdogo Arumeru yakamilika

Na Is-haka Omar ZPC Zanzibar
Tume ya taifa ya uchaguzi NEC imesema maandalizi ya uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Arumeru mashariki pamoja na ule wa madiwani katika kata nane mbalimbali hapa nchini yamekamilika.
Mwenyekiti huyo wa tume hiyo Jaji Mstaafu Damian Lubuva akizungumza jijini DSM amesema hatua mbalimbali za maandalizi zimeshakamilika, ikiwemo kuanza kusafirishwa kwa baadhi ya vifaa ambavyo vitatumika katika uchaguzi huo.
Amesema pamoja na hatua hiyo chama ambacho hakijasaini sheria ya maadili ya uchaguzi, hakitoruhusiwa kushiriki katika kampeni za uchaguzi huo mdogo ambao unatarajiwa kufanyika aprili mosi mwaka huu.
Nae Mkurugenzi wa uchaguzi wa tume hiyo Bw.Julius Mlaba amesema kampeni za uchaguzi kwa upande wa ubunge katika jimbo la arumeru mashariki zimepangwa kuanza march 9, wakati zile za udiwani katika kata nane zitaanza march 6.
Aidha amesema katika uchaguzi huo NEC itahakikisha kwamba uchaguzi huo unasimamiwa na kufanyika kwa misingi ya uhuru na haki ili kuondoa hali ya manung’uniko miongoni mwa wapiga kura kutoka vyama vya siasa .

Tuesday, January 31, 2012

Mkutano wa uchaguzi

Wajumbe wa mkutano mkuu wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi

Mwenyekiti wa Zanzibar Press Club akitoa neno la shukurani mara baada ya kumalizika kwa hutuba ya ufunguzi wa mkutano mkuu wa ZPC uliofanyika katika ukumbi wa EACROTANAL Zanzibar

Monday, November 28, 2011

Kombe la Mapinduzi Zanzibar

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema Mpango wa kuandaa Kombe la Mapinduzi Cup umelenga kukuza Michezo pamoja na kuimarisha Ujirani mwema ndani ya Mipaka ya Afrika Mashariki.
Balozi Seif ametoa kauli hiyo wakati akizindua Kamati ya Mapinduzi Cup yenye wajumbe kumi ikiongozwa na mwenyekiti wake Mohd Raza Hassan katika Ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Ocean View Kilimani Mjini Zanzibar.
Alisema mpango huu unaweza kuongeza kiwango cha Michezo ndani ya kanda hii endapo Wapenda michezo na wadau wote wataonyesha ushirikiano wao kwa kamati hii.
Balozi Seif alisisitiza kwamba Serikali haina budi kuiunga mkono Kamati hii ili kuona inafanikisha malengo iliyopangiwa.
“ Na hili nitahakikisha litatekelezwa kwa upande wa Serikali Mimi mwenyewe nitalisimamia kwa vile ndie Mtendaji Mkuu wa Serikali ”.
Alisisitiza Balozi Seif.
Aliipongeza Kamati hii kwa kuwa na wajumbe mahiri na ana matumaini ya kufanikiwa na Kamati hiyo na kuvuka kiwango cha ufanisi cha mwaka uliopita.
Akimkaribisha Balozi Seif Waziri wa Hahabi ,utamaduni, Utalii na Michezo Abdillahi Jihadi Hassan amesema Wizara ina matuimaini makubwa na Kamati hiyo kwa vile imeundwa kwa kuzingatia uwezo na uzoefu walionao.
Mapema Mwenyekiti wa Kamati ya Mapinduzi Cup Mohd Raza ameahidi kwamba Kamati yake itahakikisha inatekeleza vyema majukumu yake kwa mujibu wa matakwa ya wadau wa Michezo.
Raza alisema Kamati yao itaendelea kuzingatia zaidi huduma na burdani kwa wananchi katika mashindano ya michezo ya Mapinduzi Cup yatakayojumisha Pia Mpira wa Wavu { Netball } kwa kuzhishirikisha baadhi ya Timu za Tanzania na timu alikwa kutoka nje ya Afrika Mashariki.
Kamati hiyo iliyoundwa chini ya uwenyekiti wa Mohd Raza ina wajumbe kumi ambao ni Sherry Khamis, Ibrahim Makungu, Mwakilishi wa Jimbo la Rahaleo Nassor Jazira, Katibu Mkuu Wizara ya Habari utamaduni na Mchezo Ali Mwinyikai na Naibu wake Issa Mlingoti.
Wengine ni Ali Khalil Mirza, Taufiq Turky, Aboubakar Bagharesa pamoja na Farouk Karim ambaye ndie Mratibu wa Kamati hiyo.
Othman Khmis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Elimu ya juu Zanzibar

Taasisi za Elimu ya Juu Nchini zina wajibu wa kuhakikisha idadi ya wanafunzi wa Kike kuingia Vyuo Vikuu inaongezeka ili kukidhi mahitaji ya Jamii.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameeleza hayo kwenye mahafali ya tano ya Chuo Kikuu cha Arusha ambapo jumla ya wahitimu 600 wamemaliza masomo yao ya shahada ya kwanza na Diploma katika Fani za Biashara, elimu na Ustawi wa Jamii.
Balozi Seif alisema ongezeko hilo litaondosha kabisa pengo kubwa liliopo kati ya Wanafunzi wa Kike na Kiume katika Elimu ya Vyuo Vikuu hapa Nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuagiza Uongozi wa Chuo Kikuu cha Arusha kuongeza Mikakati madhubuti ili kuleta uwiano wa Wananfunzi wa Jinsia zote.
“ Tafiti zinaonyesha kwamba kumuelimisha Mwanamke sawa na kuwaelimisha watu kumi. Hii inamana kwamba familia itaelimika haraka iwapo kutakuwa na mmoja wa Mwanamke aliyepata elimu” Alisisitiza Balozi Seif Ali Iddi.
Alifahamisha kwamba vyuo Vikuu Vikuu lazima vishirikiane na Serikali katika kuona Dira ya Taifa ya Maendeleo ishirini ishiri
{ Vission 2020 } inafikia malengo yake.
Balozi Seif aliitaja changamoto inayowakabili wana vyuo Vikuu ni namna gain wanaweza kutumia Taaluma yao kushajiisha Sekta Binafsi katika kuibua ajira ndani ya Jamii.
Alisema hatua hiyo itakwenda sambamba na mipango ya Serikali zote mbili za kuandaa mazingira bora ya kuongeza fursa katika soko la ajira hasa kwa kundi kubwa la Vijana.
Katika risala yao iliyotolewa na Rais wa Serikali ya Wanafunzi Chuoni hapo Nd. Joshua Onyango wameiomba Serikali kuwapunguzia matatizo yanayowakabili ya Ubovu wa Bara bara, Huduma za Maji safi pamoja na Huduma za Umeme.
Wamesema matatizo hayo kwa kiasi kikubwa yanachangia kupunguza ari yao ya kujipatia Taaluma kwa utulivu ambayo ndio lengo la kuwepo kwao Chuoni hapo.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Arusha Dr. Laban Mgedi alisema lengo la chuo hicho ni kuongeza asilimia 32% ya wanafunzi wa kike Chuoni hapo.
Dr. Laban amefahamisha kwamba Afrika inahitaji wasomo wa fani tofauti wakiwemo wanawake ili kuleta Mapinduzi ya haraka ya Elimu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika Mahfali hayo pia aliweka jiwe la Msingi la Jengo la Michezo la Chuo hicho.
Jengo hilo linalotarajiwa kukamilika ujenzi wake mwezi Febuari mwakani linatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi za Kitanzania Milioni mia mbili.
Kukamilika kwa jengo hilo kutatoa afuaeni kwa wanafunzi kuwa na darasa la uhakika la masuala ya Sanaa na Utamaduni chuoni hapo.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar