Wednesday, February 29, 2012

WATU WENYE KUISHI NA ULEMAVU

Na Is-haka Omar ZPC
Kwa miaka mingi sasa ,suala la ulemavu halikuwa na umuhimu wowote katika jamii kutokana na mitizamo na imani potofu ingawa ulemavu umekuwa ukiongezeka siku hadi siku kutokana na sababu za kiuchumi,kisiasa ma kijamii.
Suala hili limeanza kuzungumzwa baada ya mwaka wa kimataifa wa watu wenye ulemavu (1981)ambapo umoja wa mataifa na jumuiya za watu wenye ulemavu dumiani zilipoanza kutetea ulemavu kama suala la haki ya binadamu.
Katika takwimu za kimataifa zinabainisha kuwa zaidi ya watu bilioni 1.5 wanapata ulemavu kila mwaka kupitia vyanzo mbalimbali vya kimaisha, lakini idadi hiyo inashamiri zaidi katika nchi zenye migogoro ya kivita kwani nchi hizo zinakuwa na watu wengi wenye ulemavu.
Tunatakiwa kufahamu maana ya ulemavu pamoja na kutofautisha aina hizo na viwango vya ulemavu,na kuelewa sababu za mtu kupata ulemavu katika kuelimisha jamii jinsi ya kujikinga na ulemavu sambamba na kuelewa changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu kidunia.
Tukumbuke kuwa ulemavu ni athari ya muda mfupi au ya kudumu inayosababishwa na hitilafu za kiwiliwili au hisia mfano uoni,usikivu,akili,kusema na kumsababishia mtu kushindwa kufanya kazi kikawaida.
Katika uchambuzi wa makala hii umebainisha aina kuu za ulemavu kuwa ni pamona ulemavu wa viungo,ulemavu wa uoni,kiziwi na matatizo ya kusema,ulemavu wa akili,albino (ulemavu wa ngozi) mwingineo kama kifafa,kichwa kikubwa mpasuko wa mdomo pamoja na ulemavu mchanganyiko ambapo mtu anakuwa na ulemavu zaidi ya mmoja.
Pia ulemavu umegawanyika katika viwango tofauti kuna ulemavu mdogo huu mtu anakuwa hitilafu au kasoro ndogo katika mwili au hisia lakini anaweza kujihudumia na kufanya kazi zote,lakini upo ulemavu wa kiasi mtu anaweza kujihudumia na kufanya kazi endapo atatumia visaidizi na mazingira yanapoboreshwa katika kiwango cha ulemavu mkubwa mtu huitaji kusaidiwa katika maisha yake yote.
Zipo sababu nyingi mtu ambazo anaweza kupata ulemavu kama kurithi,vita,utumiaji ovyo wa dawa za kulevya,magonjwa kama shinikizo la damu,kisukari,homa kali,surua,ajali,kupigwa,huduma duni kwa mama wajawazito wakati wa kujifungua na kupata mimba kwenye umri wa chini ya miaka 18 au zaidi ya miaka 35.
Changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu hapa nchini ni pamoja na kubaguliwa kijamii,kisiasa na kiuchumi mambo ambayo yakuwa vikwazo juu ya maisha yao ya kila siku na kusababisha wao kujiona kama watu ambao hawana umuhimu au haki ya kuishi kama watu wengine.
Ukosefu wa haki za msingi kama elimu,ajira na tiba zinazohusiana na wao pia ni tatizo ambalo linakua kwa kasi kubwa katika jamii yetu, licha ya kutolewa kwa elimu tofauti juu ya haki na usawa kwa watu wenye ulemavu juhudi za serikali pamoja na asasi binafsi katika kuhamasisha jamii kuondokana na dhana mbaya juu ya watu hawa ambayo wengi wanaamini kuwa watu wenye ulemavu ni moja ya jamii ambayo inahitaji msaada wa kila mara jambo ambalo si sahihi bali wanahitaji kuandaliwa mazingira mazuri ya kuweza kujitegemea wenyewe au kupewa msaada wa kielimu kama ujasilia mali ili waweze kujikimu kimaisha bila ya kutegema msaada wa mtu au taasisi fulani.
Umbali wa huduma za msingi unachangia katika kukwamisha maendeleo ya watu wenye ulemavu kwani ushindwa kufikia huduma muhimu kwa kukosa usafiri unaoendana na mazingira halisi ya watu hao,hivyo kama ni wanafunzi ushindwa kufika katika skuli au vyuo kwa muda unaotakiwa hata sehemu zao za kutafuta riziki yaani kazi halali ambayo ni haki ya msingi kwa kila mtu ,kufikia sehemu hizo upata vikwazo katika usafiri ikiwa katika daladala na aina zingine za usafiri.
Katika suala zima la kiuchumi wengi wao hukosa vyazo vya kujiingizia kipato yaani fedha na kujikuta wanashindwa kupata huduma za msingi au kushindwa kufanya biashara kutokana na hitilafu za kimaumbile walizonazo,hivyo upelekea kutomudu gharama za kununulia visaidizi vya kuwasaidia katika maisha yao ya kila siku.
Mazingira yasiyofikika nayo ni kikwazo kikubwa kwa watu hawa kwani wanashindwa kufikia huduma muhimu za kibinadamu hususani sehemu za majengo ya kwenda juu yanayojengwa na serikali pamoja na taasisi binafsi kwa ajili ya kutoa huduma za kijamii lakini ujenzi huo ,unakuwa kinyume na matarajio kwa watu hawa pamoja na jamii inayotambua haki na usawa kwa binadamu wote,kwani ujenzi huo hauzingatii miundo mbinu au matakwa ya watu wenye ulemavu kutokana na hali waliyokuwanayo ya kimaumbile unakuwa usumbufu kufikia sehemu za juu ndani ya majengo hayo kwani hapana visaidizi vya kisasa vilivyowekwa kwa ajili ya watu hawa.
Unyanyasaji na ubakaji kwa watu hawa jamii inachukulia kama sehemu ya maisha ya watu wenye ulemavu jambo ambalo si busara katika maisha halisi ya wazanzibar nchi yenye sifa za kipekee katika uso wa kidunia kwa wema,heshima,busara ,imani na hekima kwa raia wa nchi hii iliyojaa nyingi amani imetawala kila sehemu ya nchi,lakini hili tujue kuwa ni jukumu la kila mtu kusimamia na kukemea vitendo hivyo viovu ambavyo vinafanyika ndani ya jamii yetu tusitafute nani mchawi juu ya suala hili bali kukae na kutafakali kwa kina jinsi gani kumaliza tatizo hili,vipo vitendo vinavyosikitisha mfano utakuta mtu mwenye ulemavu wa akili anapewa uja uzito na mtu asiyejulikana,kweli katiba ya nchi ambayo ni sheria mama ya nchi inafanya kazi ipasavyo kwa kuwawajibisha watu wanaofanya vitendo vya uzalilisha na ubakaji kwa watu wenye ulemavu kama sheria na kanuni za nchi hazitekelezwi sasa wakati umefika kwa kila mmoja wetu kubadilika kitabia katika kusimamia na kutekeleza mambo yote yanayowahusu watu watu hawa.
Sheria ya watu wenye ulemavu( haki na fursa) na.9 ya mwaka 2006 inasema `watu wenye ulemavu wanatakiwa kuwa na fursa iliyo sawa kwa manufaa ya taifa katika nyanja zote za kijamii na katika elimu,habari,mawasiliano na mazingira ya kimaumbile kama vile lugha ya alama,tafsiri kwa visiwi,kanda,maandishi ya nukta nundu,taarifa na vipindi vinavyotokana na kompyuta,tovuti na kuweka mpangilio wa mazingira halisi kama vile nyumba,majengo,usafiri na mitaa ili waweze kuifikia.
Pia baraza la taifa la zanzibar la watu wenye ulemavu lilianzishwa chini ya kifungucha 26 cha sheria hii kwa lengo la kusimamia haki na maslahi ya watu wenye ulemavu nchini.
Kwa mujibu wa sheria hii kila jamaa wa mtu mwenye ulemavu atakuwa na wajibu wa kutoa haki na fursa kwa mtu mwenye ulemavu atakayeshindwa kufuata masharti ya kifungu (1) cha kifungu hiki atakuwa ametenda kosa,pale itakapothibitika kwa jamaa ana jhatia ya kuacha kwa makusudi kutoa haki na fursa kwa mtu mwenye ulemavu,mahkama inaweza kwa maombi kutoka kwa mtu mwenye ulemavu au baraza kuamuru kwamba haki na fursa zitolewe kwa usawa.
Mkataba wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu unatambua umuhimu wa misingi na miongozo ya sera iliyokuwemo ndani ya mpango wa vitendo wa dunia kuhusu watu wenye ulemavu na kanuni za kutoa fursa sawa katika ushawishi,uendelezaji,utengenezaji na kuthamini sera,mipango na hatua mbalimbali katika ngazi ya kimataifa,kikanda na kitaifa ili kutoa fursa sawa kwa watu wenye ulemavu.
Katika ibara ya 27 kwenye mkataba wa kimataifa unabainisha nchi zilizoridhia mkataba huo zinatambua haki ya watu wenye ulemavu kufanya kazi kwa misingi sawa na wengine hii inajumuisha haki ya kujipatia nafasi ya kumudu maisha kwa kufanya kazi walioichagua au kuibua katika soko la ajira na mazingira ya kazi yawe wazi,shirikishi na yanafikika na watu wenye ulemavu pamoja na kulinda na kukuza upatikanaji wa haki ya kufanya kazi,ikijumuisha wale waliopata ulemavu wakiwa kazini,kwa kuchukua hatua na sheria inayofaa.
Mwanaharakati wa masuala ya watu wenye ulemavu Zanzibar bw.Ali Saleh ameelezea hisia zake juu ya watu wenye ulemavu hapa nchini katika mafunzo ya siku tatu ya waandishi wa habari juu ya kutambua haki na usawa kwa watu hao amesema bado jamii inatakiwa kubadilika kitabia na kufuata kanuni na sheria za nchi ,pamoja na kutambua na kuheshimu haki za binadamu bila ya kuacha nyuma utamaduni halisi wa mzanzibar ,hayo ni mambo muhimu ya kuzingatia kwa kila mmoja wetu ili nchi yetu iwe miongoni mwa nchi zinazojali na kutambua haki na fursa kwa watu wenye ulemavu.
Bi, Zainabu Khamis Mohamed anaishi na ulemavu wa ngozi (albino) amesema suala la ulemavu ni kasoro ndogo za kibinadamu zinazoweza kutokea kwa binadamu yeyote,hivyo jamii iwashirikishe katika masuala mbalimbali nao wanaweza kushiriki katika ujenzi wa taifa kama watu wengine ni muhimu kuondokana na imani potofu kuwa watu hao hawawezi kufanya kazi au kupata elimu vitu ambavyo ni msingi wa maisha ya kila mtu.
Aidha ametoa wito kwa serikali pamoja na taasisi binafsi kushirikiana katika kuwawezesha kiuchumi ili waweze kujiajiri wenyewe kwani kufanya hivyo kutawasaidia katika masuala mbalimbali ya kujikwamu kimaisha na kuondokana na umasikini.
Kama Mwandishi wa makala hii nina machache kwa jamii kweli yapo matukio mengi ya kusikitisha na kutisha wanayofanyiwa watu wenye ulemavu,lakini mbaya zaidi vyombo vyenye dhamana ya sheria vipo kimya wakati sheria na mkataba wa kimataifa ipo lakini wahusika wanaofanya matukio hayo hawawajibishwi,je kama sheria hazitekelezwi jamii zilizochoka na unyanyasaji na uonevu zitakuwa na imani au uzalendo juu ya nchi yao, tubadilikeni kwani suala la ulemavu si la mtu au watu Fulani kila mtu ni mlemavu mtarajiwa kama si leo basi kesho yaweza ukawa mlemavu wahenga walinena “kama ujafa ujaumbika ”methali hii tuitafakali kisha turudi katika misingi ya dini zetu bila ya kuacha nyuma utamaduni na uhalisia wa maisha yetu ya kila siku.
Ushauri wangu kwa serikali sasa naweza kusema kwamba wakati umefika wa serikali kukunjua mbawa zake katika jamii na kusimamia ipasavyo haki ma fursa kwa watu wenye ulemavu ili nao,waweze kuondokana vilio vya muda juu ya ubaguzi,mateso,machungu yaliyopelekea kukata tamaa kwa walio wengi,ni muhimu kufikiria zaidi juu ya uwepo wa watu hawa wenye uwezo mkubwa wa kiutendaji wakiwezeshwa na kupewa mbinu za kujikwamua pia washirikishwe katika mambo mbalimbali ya kitaifa na kijamii.

Ufafanuzi unahitajika juu ya dhana nzima ya serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar

Mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa unaoendelea kufuatwa Zanzibar hivi sasa unafaa kuigwa na Mataifa mengine Duniani katika harakati za kudumisha Demokrasia ndani ya Jamii.
Katibu Mtendaji wa Mpango wa Nchi za Kiafrika kujitathmini Kiutawala Bora { APRM } Tanzania Bibi Rehema Twalib alisema hayo wakati Ujumbe wa Uongozi wa Bodi ya Mpango huo ulipokuwa ukiwasilisha Ripoti ya Utawala Bora na Mpango Kazi.
Ripoti hiyo wameiwasilisha kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Bibi Rehema alisema dhamira inayopaswa kuchukuliwa hivi sasa ni kuona namna gain uelewa unajengwa kwa Viongozi na Wananchi katika kujuwa mfumo huo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
“ Zipo dalili zinazoonyesha kwamba baadhi ya Viongozi wakiwemo watedaji wa Serikali na hata Wananchi bado hawajaufahamu mfumo huo”. Alisema Bibi Rehema.
Katika suala la Kiuchumi Bibi Rehema alifahamisha kwamba juhudi zinahitajika katika kuhamasisha Sera katika kuharakisha Maendeleo ya Jamii.
Alieleza kuwa Sekta ya Viwanda ambayo hutoa ajira kwa kundi kubwa la Wananchi hasa Vijana bado haijafanya vyema na vizuri likaimarishwa sambamba na uwekezaji Vitega Uchumi.
Akizungumzia suala la Kodi Katibu Mtendaji huyo wa APRM alitahadharia kuachwa kwa tabia inayoendelezwa na baadhi ya Watendaji wa Serikali kuwakatisha Tamaa Wafanyabiashara katika kazi zao.
Bibi Rehema alisema tabia ya watendaji hao kuwatoza kodi mara mbili wafanyabiashara kwenye Biashara zao kati ya Zanzibar na Tanzania Bara ni kuendeleza kero zinazoweza kuepukwa.
Kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Nchi nyingi zimekumbwa na migogoro hasa ya Kisiasa na hata ya ardhi kwa sababu ya kushindwa kuweka utaratibu mzuri wa kuiepuka migogoro hiyo.
Balozi Seif alisema Zanzibar imekuwa na uzoefu wa migogoro ya kisiasa kwa muda mrefu tokea miaka ya 50 na hili ndio lililopelekea Wananchi wake kutafuta mbinu za kuondokana na mfumo huo uliodumisha ustawi wa Maisha yao.
Hata hivyo alisema kasoro ndogo ndogo bado zipo lakini ikitokea kuchomozwa kwa migogoro ya kisiasa hapa Tanzania ni ya kujitakia wenyewe kwa vile taratibu sahihi za kuendesha Utawala Bora tayari zimeshawekwa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliipongeza Taasisi hiyo ya Mpango wa Nchi za Kiafrika kujitathmini Kiutawala Bora
{ APRM } kwa kufanya kazi kubwa ya kuelimisha Jamii za Kiafrika juu ya Utawala Bora.
Ziara ya Ujumbe huo imehusisha pia matayarisho ya ujio wa Uongozi wa Juu wa Taasisi hiyo ya Mpango wa Nchi za Kiafrika kujitathmini Kiutawala Bora {APRM } ambao unatazamiwa kufanya ziara Maalum hapa Zanzibar kuanzia Tareha 2/3/2012 hadi 22/3/2012.
Ukiwa hapa Zanzibar Ujumbe huo utakaoongozwa na Bibi Marista Seruma utakutana na Viongozi wa Juu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Watendaji na hata wawakilishi wa Taasisi na Jumuiya Tofauti.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi ameagiza kusitishwa kwa ujenzi wahoteli katika kijiji cha Nungwi, wilaya ya Kaskazini Unguja

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameagiza kusitishwa mara moja kwa shughuli zozote za ujenzi wa Maradi wa Hoteli katika eneo la Nungwi Mashariki lenye ambalo linaukubwa wa Hekta 30.5.
Agizo hilo amelitoa wakati wa ziara yake ya siku tatu ya kutembelea Miradi ya Maendeleo na ile ya Kijamii ndani ya Mkoa wa Kaskazini Unguja .
Balosi Seif alisema zipo dalili za ujanja zinazoonekana kufanywa na Maafisa wachache na kupelekea mgongano na malalamiko ya umiliki wa eneo hilo kufuatia kufuta kwa mkataba wa ujenzi wa Mradi wa Kitalii wa Kampuni ya Spice Island kwa madai ya kukiuka masharti.
Balozi Seif alikemea tabia inayofanya na baadhi ya Watendaji wa Idara ya Ardhi ambayo inawabughudhi Wawekezaji na hatimae kuitia aibu Serikali.
“ Inashangaza kuona Idara ya Ardhi inamfutia mkataba muekezaji mmoja kwa kushindwa kutekelezaa mkataba ndani ya miaka miwili, lakini idara hiyo hiyo kumpa mwekezji mwengine kwa zaidi ya miaka saba bila ya kumvunjia ”. Balozi Seif alisema lipo jambo katika mradi huo.
“ Kuanzia sasa nasema sitaki kuona shuguli yoyote ya ujenzi inaendeshwa katika eneo hili hadi Serikali Kuu itakapofanya maamuzi baada ya kufanya utafiti wa kina kuhusiana na mgongano huo”. Balozi Seif alikuwa akimuagiza Afisa wa Ardhi Bwana Sanani Baraka kufanya kutekeleza agizo hilo.
Kwa upande waoWananchi wa Kijiji cha Nungwi wameelezea masikitiko yao kutokana na mgongano huo unaopelekea kucheleweshewa maendeleo yao ya Kijamii kupitia makubaliano ya Mradi wa mwanzo ambao tayari ulikuwa umeshakubalika baina yao na mwekezaji wa awali.
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliweka jiwe la msingi la Afisi ya Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo cha Mkwajuni na kuwapongeza kwa uamuzi wa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2010 ya kuendeleza Vikundi vya Ushirika.
Balozi Seif alisema Wanachama hao bado wanahitaji kukuza Chama chao ili kukijengea mazingira mazuri ya kujipatia mahitaji yao.
Baadaye Balozi Seif aliweka jiwe la msingi la Jengo jipya la Skuli ya Kidagoni iliyoko ndani ya Jimbo La Nungwi.
Ujenzi wa Skuli hiyo umekuja kufuatia Watoto wa Vijiji vya Kidagoni na Mwanguo kufuata Elimu katika masafa marefu.
Balozi Seif alisema nia nzuri ya Wazee wa Vijiji hivyo ni hatua ya msingi ya kuwajengea hatma njema ya Kielimu Watoto wao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif amewaomba Wananchi hao kuwa na subra kutokana na changa moto wanaopambana nazo za bara bara, maji safi na Kituo cha Afya na kusema Serikali inaangalia njia za kuyatatua matatizo hayo.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Tuesday, February 28, 2012

Zanzibar kuendeleza ushirikiana wa kielimu na Sudan

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahakikisha kwamba uhusiano kati yake ya Sudan inaendelea kuimarika wakati wote.
Balozi Seif alisema hayo wakati wa mazungumzo yake na Balozi Mpya wa Sudan Nchini Tanzania Dr. Yassir Mohd Ali aliyefika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kujitambulisha.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Zanzibar na Sudani zimekuwa na uhusiano wa Kihistoria wa muda mrefu hasa katika Sekta ya Elimu.
Alisema Wanafunzi wengi wa Zanzibar wamekuwa wakipata Elimu ya Juu katika vyuo mbali mbali kwenye fani za lugha na Sheria ya Dini ya Kiislamu.
Balozi Seif alisisitiza kwamba Taaluma hiyo inakwenda sambamba na Walimu wa Sudan kutoa Taaluma hapa Zanzibar katika vyuo tofauti hasa katika somo la Dini na Lugha ya Kiarabu.
“ Uwepo wa Chuo Kikuu cha Elimu Chukwani ambacho kiko chini ya udhamini wa Taasisi ya Africa Muslim Agency ya Nchini humo ambacho hivi karibuni nilikuwa mgeni rasmi katika mahfali ya 11 ya chuo hicho ni ushahidi wa uhusiano huo ”. Alisema Balozi Seif.
Mapema Balozi Mpya wa Sudan Nchini Tanzania Dr. Yassir Mohd Ali
Aliahidi kuendeleza uhusiano huo ambao utakuwa chachu ya Umoja Miongoni mwa Mataifa ya Bara la Afrika.
Dr. Yassir alisema Afrika hivi sasa inapaswa kujikita zaidi katika kujiletea Maendeleo na kuachana na migogoro inayoleta migongano miongoni mwa Wananchi wake.
Akigusia mikakati ya kupunguza migogoro ya kisiasa hasa katika Nchi yake Balozi Yassir alisema Uhuru wa Sudan ya Kusini umepunguza joto la Kisiasa kati ya pande hizo mbili.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikuwa na mazungomzo ya Ujumbe wa Watu wawili kutoka Kampuni ya Camden Hospitality Group inayojishughulisha na Miradi ya Hoteli za Kimataifa kutoka Nchini Marekani.
Katika mazungumzo yao Kiongozi wa Ujumbe huo Bwana Munir Walji alisema ziara yao imekuja kufuatia mazungumzo yao ya mwaka uliopita kuhusu uwekezaji wa Miradi ya Hoteli za Kimataifa za nyota Tano pamoja na huduma nyengine za Utalii.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Sunday, February 26, 2012

Washiriki wa mafunzo ya habari za uchokonozi

Ni baadhi ya washirriki kutoka Tanga Press Club wakati wa mafunzo ya habari za uchokonozi yaliyofanyika Zanzibar hivi karibuni
Mshiriki wa mafunzo ya habari za uchokonozi akifafanua jambo


Saturday, February 25, 2012

Kampeni ya maliza malaria yapamba moto Zanzibar

Na Is-haka Omar ZPC
Kitengo cha kupambana na malaria Zanzibar kimeanza kazi za usajili wa kaya ikiwa ni matayarisho ya ugawaji wa vyandarua unaotarajiwa kufanyika mapema mwezi ujao.
Kazi hizo zilizoanza jana zitaendelea kwa muda wa siku tatu ili kupata idadi sahihi ya kaya zitakazopatiwa vyandarua ambapo kwa mujibu wa kitengo hicho kiasi vyandarua laki saba vitagaiwa bure kwa wananchi wa Unguja na Pemba..
Meneja wa kitengo cha kupambana na malaria Bw.Abdalla Suleiman amesema kiasi ya vijana elfu mbili wa wilaya zote wamepatiwa mafunzo ya usajili wa kaya na kusambaza vyandarua kwa wananchi.
Amefahamisha hatua hiyo itasaidia kufanikisha ugawaji wa vyandarua na kutoa wito kwa wananchi kutodharau usajili huo ili kila kaya ipate chandarua kwa lengo la kutomeza malaria Zanzibar.

Balozi Seif afanya mazungumzo na Balozi wa EU Tanzania

Na Is-haka Omar ZPC
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amefanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Ulaya (E.U) nchini Tanzania Bw.Filiberto Ceriani.
Katika mazungumzo yao viongozi hao walielezea haja ya kuongeza ushirikiano kati ya pande hizo mbili na Bw.Filiberto amesema umoja wa ulaya umeandaa mpango wa kuzijengea uwezo jumuiya na taasisi za kiraia utakaogharimu karibu Euro milioni tatu.
Amesema mpango huo utaenda sambamba na utowaji wa mafunzo kwa watendaji wa sekta ya sheria ili kuwajengea mazingira bora ya uwajibikaji sekta hiyo.
Nae Balozi Seif amesema Zanzibar inaendelea kupiga hatua za maendeleo kufuatia uendeshaji wa mfumo wa serikali ya umoja wa kitaifa.
Hata hivyo Balozi Seif amesema bado yapo maeneo muhimu ya huduma za kijamii kama maji, elimu na afya hayajafikia kiwango kilicholengwa.
Hivyo amesema msaada zaidi unahitajika kutoka kwa taasisi na washirika wa maendeleo juhudi hizo za serikali za kuwaletea maendeleo wananchi.

Msumbiji yaitaka Tanzania kufukiria njia ya kurudisha vikao vya pamoja

Na Is-haka Omar ZPC
Msumbiji imeiomba Tanzania kufikiria uwamuzi wa kurejeshwa tena utaratibu wa kuwa na vikao vya pamoja kati ya pande hizo mbili ambao ulilenga zaidi kuimarisha ujirani mwema.
Ombi hilo limetolewa na Balozi wa Msumbiji nchini Tanzania Bw.Zakaria Kupella wakati alipofanya mazungumzo na makamu wa pili wa rais wa zanzibar balozi Seif Ali Iddi hapo ofisini kwake vuga mjini Zanzibar.
Amesema tanzania ilikuwa mstari wa mbele katika kusaidia ukombozi wa mataifa ya bara la afrika ikiwemo jirani yake Msumbiji hivyo ni vyema vikao vya ushirikiano vikafufuliwa kwa nia ya kulinda umoja na udugu wa sehemu hizi mbili.
Amesistiza kwamba yapo maeneo mengi ambayo wananchi wa pande hizo mbili wamekuwa wakishirikiana pamoja hasa ikizingatiwa kwamba nchi hizo zimepakana.
Balozi huyo amesema ni vyema ukaandaliwa utaratibu wa kuyaunganisha makundi ya vijana wa pande hizo mbili kujenga taifa katika mpango wa kujitolea.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema uhusiano wa pande hizo mbili unafaa uelekezwe zaidi katika uchumi badala ya siasa ambapo ameiomba msumbiji kufikira wazo la kutoa wataalamu kuja zanzibar katika kutoa elimu katika sekta ya uvuvi wa kamba.
Balozi Seif amesema dunia imeshuhudia kiwango kikubwa cha bidhaa ya kamba inayozalishwa msumbiji na kusafirishwa nje ya nchi na kuipatia kipato kikubwa nchi hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa mjini azuwiya ujenzi katika wilaya yake

Na Is-haka Omar ZPC
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Bw.Abadalla Mwinyi Khamis ametoa agizo la kuzia uuzaji wa viwanja na ujenzi wa aina yoyote katika eneo ambalo wananchi wa shehia ya mbuzini wanalihitaji kulitumia kwa ujenzi wa miradi ya kijamii.
Amesema tabia inayofanywa na baadhi ya watu kuuziana viwanja kiholela si utaratibu unaofaa hivyo ameuagiza uongozi wa wilaya ya Magharibi kushirikiana na wananchi wa eneo hilo kuliomba eneo hilo kwa wizara ya ardhi ili kupata umiliki na kulitumia kwa malengo yao.
Ametoa agizo hilo wakati wa ziara huko mbuzini kufuatia malalamiko ya wananchi kuhusu kuwepo kwa baadhi ya viongozi kuuza viwanja kwenye neo hilo.
Nao wananchi wa Mbuzini wameelezea kusikitishwa na vitendo vinavyofanywa na baadhi ya viongozi kuuza viwanja ovyo pamoja na kuutupia lawama uongozi wa jimbo kwa kushindwa kufuatilia suala hilo.
Wakati huo huo mkuu huyo wa mkoa amefanya ziara shehia ya Fuoni Pangawe kuona uharibifu wa mazingira unaofanywa kwa uchimbaji mchanga na kuutaka uongozi wa shehia hiyo kuimarisha polisi shirikishi jamii ili walinde maeneo yao.

Friday, February 24, 2012

Kiongoni watakiwa kuinua sanaa

Na Is-haka Omar ZPC
Katibu Mkuu Wizara ya Kazi,Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika Bi.Asha Ali Abdallah amekitaka kikundi cha sanaa cha skuli ya Kiongoni kuendeleza sanaa ya ngoma kwani vipaji vikiendelezwa hupelekea kuwa sehemu ya kujifunza na kupata ajira.
Hayo ameyaeleza wakati wa kukabidhi fedha taslimu sh.laki tano kwa kiongozi wa kikundi hicho cha sanaa huko ofisini kwake Mwanakwerekwe.
Amesema lengo la kutolewa kuwa fedha hizo ni kuendeleza kikundi hicho kiweze kukua kisanaa na kuinua vipaji vya wasanii.
Bi.Asha amefahamisha kuwa msaada huo umetolewa kufuatia ahadi alizotoa makamo wa pili wa rais Mhe.Balozi Seif Ali Idd katika uzinduzi wa soko la jumapili (sunday market) huko michenzani.
Nae mwalimu wa kikundi hicho Bw.Shaabani Naim Suleiman ametoa shukrani zake kwa makamo wa pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi kwa kutimiza ahadi yake pamoja na kuahaidi kuwaendeleza wasanii.
Kikundi hicho kima wanafunzi 15 na viongozi 3 na wanajishughulisha na ngoa za msewe,chaso na kurungu.
Pamoja na hayo kazi kubwa ya kikundi hicho ni kutoa elimu kwa jamii juu ya mambo mbalimbali kupitia sanaa ya ngoma ikiwemo utunzaji wa mazingira ,dawa za kulevya na ukimwi.

Waandishi watakiwa wawe wafuatailiaji wa kina juu ya matukio na masuala yawahusuo watu wenye kuishi na ulemavu

Na Is-haka Omar ZPC
Waandishi wa habari nchini wametakiwa kushiriki kikamilifu katika kufuatilia kwa kina na kuandika habari na matukio mbalimbali ya watu wenye ulemavu ili waweze kupata haki zao za msingi kisheria.
hayo yameelezwa na mwenyekiti wa bodi kutoka ofisi ya umoja wa watu wenye ulemavu Zanzibar Bw.Ali Omar Makame wakati akifungua mafunzo ya siku 3 huko katika ukumbi wa jumuiya hiyo weres kwa waandishi wa habari juu ya kutambua haki za msingi za watu wenye ulemavu kisheria.
Amesema waandishi wa habari watumie taaluma yao katika kuelimisha jamii kwa kuandika habari na kufichua maovu wanayofanyiwa watu wenye ulemavu ili nao wapate haki zao za msingi kama watu wengine katika jamii.
Aidha Bw.mMakame amefahamisha kuwa watu wenye ulemavu wanatakiwa kushirikishwa katika mambo mbalimbali yanayowahusu hususani kijamii,kiuchumi na kisiasa.
Nae mwezeshaji katika mafunzo hayo bw.ali saleh amesema watu wenye ulemavu katika mkataba wa kimataifa wanatakiwa kuwa na fursa iliyo sawa kwa manufaa ya taifa katika nyanja zote za kijamii na katika hali yoyote inayojumuisha upatikanaji wa elimu, habari, mawasiliano na mazingira ya kimaumbile.
Bw.Saleh amesema kuwa sheria namba 9 ya mwaka 2006 ya Zanzibar ya watu wenye ulemavu inamapungufu katika suala zima la utekerezwaji kwani walengwa wa sheria hiyo hawapatiwi haki zao kwa mujibu wa sheria inavyoeleza hususani katika ujenzi wa majengo ya serikali pamoja na asasi za kiraia hawazingatii miundo mbinu inayoendana na mazingira halisi ya watu wenye ulemavu na kusababisha usumbufu mkubwa bindi wanapotaka kupata huduma mbalimbali za kijamii.

Serikali yatakiwa kulipatia ufumbuzi tatizo la ubovu wa barabara ya Kinuni-Unguja

Na Is-haka Omar ZPC
Wananchi wa shehia ya Kinuni wameiomba serikali kuwatatulia tatizo la ubovu wa barabara ya eneo hilo ili kuwaepushia usumbufu wanaopata.
Wamesema wakati umefika kwa serikali na taasisi binafsi kuweka mikakati mbalimbali ili kuona barabara za maeneo mbalimbali ikiwemo ya eneo hilo zinajengwa na kuimarishwa kwa lengo la kuwaondolea wananchi usumbufu katika utekelezaji wa shughuli zao za kila siku.
Wakizungumza na waandishi wa habari hizi wamesema wamekuwa wakikabiliwa na usumbufu mkubwa pale wanapokuwa safarini kutokana na ubovu wa barabara hiyo jambo ambalo linawaresha nyuma maendeleo yao.
Hivyo wamesema kukosekana kwa barabara ya uhakiki katika shehia hiyo kunasababisha kutofanyika shughuli zao kwa ufanisi zaidi

ZAWA yatakiwa kulipatia ufumbuzi tatizo la maji Chumbuni

Na Is-haka Omar ZPC
Mamlaka ya maji zanzibar ZAWA imeombwa kulitafutia ufumbuzi tatizo la maji safi na salama linalowakabili kwa muda mrefu wananchi wa maeneo ya chumbuni.
Wakizungumza na waandishi wa habari hizi wananchi wa shehia hiyo wamesema tatizo hilo linarejesha nyuma shughuli zao za kujiletea maemdeleo na kuathiri maisha yao ya kila siku.
Wamesema maji wanayoyategemea hivi sasa ni ya kisima cha Chumbuni na Masjdi Raudha ambayo wanalazimika kulipia shilingi 50 kwa kila ndoo.
Hivyo wameitaka mamlaka hiyo kulishughulikia tatizo hilo kwa umakini kwa vile maji ni huduma muhimu katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za jamii

Miti elfu moja yatarajiwa kupandwa ikiwa ni miongoni za njia bora za kuhifadhi misitu Zanzibar

Na Is-haka Omar ZPC
Kiasi ya miti elfu moja inatarajiwa kupandwa katika sehemu za wazi za kijiji cha Jendele hadi Cheju ikiwa ni harakati za kuimarisha hifadhi ya misitu na utunzaji wa mazingira katika vijiji hivyo.
Mradi huo unatarajiwa kutekelezwa na kamati ya uhifadhi wa misitu ya asili ya cheju pembezoni mwa barabara ambapo hivi sasa wanasubiri utekelezaji wa ujenzi wa barabara inayounganisha vijiji hivyo uanze ili kuona maeneo muafaka yatakayotumika.
Sheha wa shehia ya cheju Bw.Kassim Suleiman Mdunga amesema wameshatoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa idara ya mistu ili kupatiwa msaada na maelekezo zaidi juu ya zoezi hilo.
Amefahamisha kuwa shehia hiyo imeamua kupanda miti ya miembe boribo ambayo ni miongoni mwa mimea inayoanza kupotea kutokana na ongezeko la watu kujihusisha na shughuli za ukataji miti kwa ajili ya kujiongezea kipato na matumizi ya kijamii.
Kwa upande wake sheha wa shehia ya jendele Bw.Ame Makame Rajab ameiomba serikali kuhamasisha jamii katika kutafuta mbinu mbadala zitakazosaidia kupumguza vitendo vya ukataji miti kiholela katika shehia hizo.

Oman yasaidia Zanzibar kimatibabu

Na Is-haka Omar ZPC
Serikali ya Oman imekusudia kutoa msaada wa matibabu nje ya nchi kwa watoto kuanzia mwaka mmoja hadi miaka kumi na sita wanaosumbuliwa na ugonjwa wa moyo.
Waziri wa afya Mhe.Juma Duni amesema kuwa wagonjwa hao watapelekwa katika hospitali ya Narayana nchini india kuanzia mwazoni mwa mwezi ujao kwa gharama zitakazotolewa na serikali ya oman ambapo mgonjwa mmoja anakisiwa kugharimu kiasi ya dola elfu nne hadi tano.
Akizungumza na waandishi wa habari amesema hatua hiyo itakuwa ya kuendela ikiwa ni juhudi ya wizara hiyo katika kutafuta ufadhili wa matibau ya watoto ambapo katika hatua ya awali watoto kumi hadi ishirini watasafirishwa kwa ajili ya matibau zaidi.
Mhe Duni amefahamisha kuwa timu ya madaktari watatu kutoka hospitali ya Narayana wanaendelea na zoezi la kuchunguza watoto hao kisiwani pemba na kwa unguja watoto 73 wamegundulika kuhitaji matibabu zaidi.
Hivyo ameishukuru serikali ya oman kwa ufadhili huo baada ya kuelewa tatizo hilo ikiwa ni juhudi za kusadia kuimarisha ustawi wa afya za watoto nchini.

Skuli ya Kisiwandui kufaidika na mtandao wa teknolojia

Na Is-haka Omar ZPC
Mbunge wa jimbo la kikwajuni Mh.Hamad Yussuf Masauni amekabidhi hundi ya shilingi milioni mbili kwa kampuni ya milenium enginearing ya Dar-es-salaam kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha teknohama ndani ya jimbo hilo.
Akikabidhi hundi hiyo amesema ujenzi huo utajengwa kwa awamu ambapo awamu ya kwanza itagharimu shilingi milioni tano ambacho kitawasaidia wananchi kitajengwa ndani ya eneo la skuli ya Kisiwandui kitawawezesha vijana kujiingiza katika mtandao wa sayansi na teknologia.
Akizungumzia suala la uimarishaji wa barabara za ndani ya jimbo hilo mh masauni amesema wamo mbioni kuzifanyia matengenezo ili kuziweka katika hali ya kuridhisha.
Nae mhandisi kutoka kampuni hiyo Bw Ali Bakari Ali amesema kampuni hiyo inashughulikia miradi mbali mbali ya maendeleo ya wananchi ambapo kwa hapa watajenga kituo hicho cha teknohama ili kuendeleza elimu nchini.
Aidha amewataka wananchi kufuata taratibu za kisheria wakati wanapotaka kujenga pamoja na kupata ushauri wa kitaalamu ili kuepusha usumbufu unaoweza kujitokeza .

Wednesday, February 22, 2012

JUMMAZA yakusudia kuziweka nyumba za maendeleo Kilimani kuwa safi

Na Is-haka Omar ZPC Zanzibar
Katibu wa jumuiya ya uhifadhi wa mazingira na maendeleo Zanzibar JUMMAZA Bw Ramadhan Fadhil amesema jumuiya hiyo imedhamiria kulifanya eneo la nyumba za maendeleo kilimani kuwa katika hali ya usafi na salama .
Akizungumza na waandishi wa wahabari wa vyombo mbalimbali huko kilimani amesema hatua hiyo imekuja kufuatia eneo hilo kuwa katika hali isiyoridhisha na kuhatarisha maisha ya wakaazi wa eneo hilo .
Bw Ramadhan amesema tayari jumuiya yake imeshaanza kazi ya kuondoa taka zilizomo pembezoni mwa nyumba hizo na kusafisha majani yaliyopo kweye eneo hilo .
Amesema baada ya hatua hiyo wanatarajia kusafisha mitaro na kuchukua taka nyumba hadi nyumba zoezi ambalo linatarajiwa kuwa la kudumu
Aidha ameiomba serikali na taasisi binafsi kuunga mkono jitihada za jumuiya hiyo iweze kufanikisha kazi ya kuweka mazingira safi na salama

ZAFEPED yatakiwa kubuni mbinu mbadala za kuwasaidia wananchi kutokana na umasikini

Na Is-haka Omar ZPC Zanzibar
Mkuu wa wilaya ya kusini Bw Haji Makungu Mgongo amewataka wanajumuiya ya kupambana na umasikini na uharibifu wa mazingira ZAFAPED kubuni mbinu mbali mbali zitakazowasaidia wananchi kuondokana na umasikini .
Akizungumza na viongozi wa jumuiya hiyo ofisini kwake amesema wananchi wengi wa wilaya ya kusini wanatengemea misitu katika kupata ajira hali inayosababisha uharibifu mkubwa wa mazingira .
Amesema ili wananchi waondokane na tatizo la uharibifu wa mazingira ipo haj ya kutoa elimu kuondokana na uharibifu wa mazingira ikiwemo misitu katika wilaya hiyo tatizo ambalo limedumu kwa muda mrefu .
Nae Mkurungezi wa jumuiya hiyo Bw. Faida Khamisi Ali amesema lengo kuu la jumuiya hiyo ni kuwapatia wananchi elimu na mbinu za kupambana na umasikini .
Jumuiya hiyo inafanya kazi zanzibar katika shehia za wilaya ya kusini ikiwemo mtende ,pete na kajegwa kwa kupitia mradi wa hima na Care tanzania ambapo mradi huo utakuwa wa mienzi sita .

Maalim Seif awataka watendaji wa chama cha CUF kuwa karibu na wanachama wao

Na Is-haka Omar ZPC Zanzibar
Katibu mkuu wa chama cha wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad amewataka watendaji wa chama hicho ngazi ya wilaya kufanya kazi kwa karibu na wanachama ikiwa ni hatua muhimu katika kukijenga chama chao.
Amesema watendaji hao wana nafasi kubwa katika kukijenga na kukiimarisha chama hicho, ikizingatiwa kuwa wao ndio wenye mawasilianao ya karibu zaidi na wanachama pamoja na wananchi kwa ujumla.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ametoa wito huo leo katika hoteli ya mazsons shangani mjini zanzibar, wakati akifungua semina elekezi kwa wenyeviti na makatibu wa wilaya wa chama cha CUF, yenye lengo la kujadili dhana ya utumishi wa umma.
Amewataka wajumbe wa mkutano huo kuijadili dhana hiyo kwa umakini mkubwa, kwa kuzingatia zaidi maslahi na maendeleo ya chama hicho, sambamba na kuhimiza suala la uwajibikaji kwa viongozi wa ngazi zote za chama.
Semina hiyo imehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa chama hicho wakiwemo wenyeviti na makatibu wa wilaya kutoka wilaya zote za unguja na Pemba.

Mkuu wa Wilaya awataka watendaji wa wilaya ya mkoani kushirirki ipasavyo katika kamapeni ya chanjo ya Surua

Na Is-haka Omar ZPC Zanzibar
Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Bw. Jabu khamis Mbwana amewataka watendaji wa Wilaya za Mkoani Pemba kushirikiana ipasavyo katika kukabiliana na ugonjwa wa surua .
Mkuu huyo wa wilaya ya mkoani amesema viongozi wa afya ,masheha wa shehia nane za wilaya hiyo, madiwani na viongozi wa vyama wanapaswa kushirikiana pamoja katika kulikabili tatizo la ugonjwa wa surua katika shehia hizo.
Ndugu Mbwana ametoa wito huo huko ukumbi wa Umoja ni Nguvu wakati akizungumza na viongozi na walimu wakuu wa skuli saba za shehia hizo ambazo zinakabiliwa na mripuko wa maradhi ya surua katika shehiya hizo.Shehia za Mizingani,Mgagadu,Ngwachani,KisiwaPanza,Chokocho,stahabu,wambaa, na shumbageni zinaelezwa kukumbwa na mripuko mkubwa ugonjwa wa surua katika kisiwa cha Pemba. Ndugu Mbwana amefahamisha kuwa jambo lililopelekea kutokea kwa mripuko wa maradhi hayo ni wananchi wakati wa chanjo iliyopita kudharau kuwapeleka watoto kupatiwa chanjo licha ya elimu kutolewa kabla ya chanjo hiyo.
Pamoja na hayo amesema kutokana na tatizo hilo wizara ya afya kwa kushirikiana na serikali ya wilaya ya mkoani inakusudia kutoa chanjo hiyo.

NEC maandalizi ya uchaguzi mdogo Arumeru yakamilika

Na Is-haka Omar ZPC Zanzibar
Tume ya taifa ya uchaguzi NEC imesema maandalizi ya uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Arumeru mashariki pamoja na ule wa madiwani katika kata nane mbalimbali hapa nchini yamekamilika.
Mwenyekiti huyo wa tume hiyo Jaji Mstaafu Damian Lubuva akizungumza jijini DSM amesema hatua mbalimbali za maandalizi zimeshakamilika, ikiwemo kuanza kusafirishwa kwa baadhi ya vifaa ambavyo vitatumika katika uchaguzi huo.
Amesema pamoja na hatua hiyo chama ambacho hakijasaini sheria ya maadili ya uchaguzi, hakitoruhusiwa kushiriki katika kampeni za uchaguzi huo mdogo ambao unatarajiwa kufanyika aprili mosi mwaka huu.
Nae Mkurugenzi wa uchaguzi wa tume hiyo Bw.Julius Mlaba amesema kampeni za uchaguzi kwa upande wa ubunge katika jimbo la arumeru mashariki zimepangwa kuanza march 9, wakati zile za udiwani katika kata nane zitaanza march 6.
Aidha amesema katika uchaguzi huo NEC itahakikisha kwamba uchaguzi huo unasimamiwa na kufanyika kwa misingi ya uhuru na haki ili kuondoa hali ya manung’uniko miongoni mwa wapiga kura kutoka vyama vya siasa .