Tuesday, August 20, 2013

Dk.Shein apongeza PBZ

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesifu hatua zilizochukuliwa katika kuiimarisha Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) ikiwa ni pamoja na utoaji mikopo kwa wajasiriamali na kujiunga na mitandao mbali mbali kwa ajili ya kutoa huduma za kutuma fedha kwa wana Diaspora.

Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipokutana na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugrnzi wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), na kufanya nao mazungumzo huko Ikulu mjini Zanzibar.

Katika maelezo yake Dk. Shein alieleza kuwa mafanikio makubwa yameweza kupatikana kutokana na uongozi thabiti wa benki hiyo sambamba na umakini wa vionghozi wa Serikali kuu.

Alieleza matumaini yake makubwa katika benki hiyo kutokana na na hatua mbali mbali inazozichukua katika kujiimarisha hali ambayo itaimarisha uchumi na maendeleo ya Zanzibar na watu wake.

Kwa upande wa kujiunga na mitandao mbali mbali kwa ajili ya kutoa huduma za kutuma fedha kwa wana Diaspora, Dk. Shein alipongeza hatua hiyo na kusema kuwa italeta maendeleo makubwa na kuweza kutimiza azma ya serikali anayoiongoza.

Aliwataka wajumbe hao kutorudi nyuma na badala yake waendelee na juhudi zao hizo huku akieleza kuwa serikali imedhamiria kuwasaidia wajasiariamali na ndio maana ina mpango kabambe wa kuanzisha Mfuko maalum utakaowasaidia huku akipongeza azma ya PBZ ya kuwasaidia wajasiriamali.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza azma ya Serikali katika kuwasaidia wakulima kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa chakula na tayari imeshaanza kupunguza ruzuku pembejeo za kilimo zikiwemo matreka, dawa, mbegu, mbolea na kusisitiza mpango wa Serikali wa kununua matrekta 20 mwaka huu.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alipongeza juhudi za PBZ katika kuanzisha huduma za kibenki kwa njia ya mitandao ya simu za mkononi pamoja na internet, huduma ambayo itarahisiha upatikanaji wa huduma zake kwa urahisi zaidi.

Nao Wajumbe wa Bodi hiyo ya Wakurugenzi wa PBZ, walieleza maendeleo yaliopatikana na Benki hiyo baada ya uimarishaji wake na kueleza ukuaji wa amana za wateja na rasiliamli sambamba na ukuaji wa kikopo kwa wateja.

Bodi hiyo ilieleza kuwa PBZ imeweza jinsi ilivyofanyia matengenezo matawi yake ikiwa ni pamoja na kujenga jengo jipya la ChakeChake na kuweka mtandao wa ATM ili kupunguza foleni.

Aidha, Bodi hiyo ilieleza kuwa tayari imeshafungua matawi kutoka matawi matatu hadi matawi tisa na vituo vine katika sehemu mbali mbali, kuanzia mwaka 2010 hadi 2012.

Kwa upande wa huduma za benki ya Kiislamu uongozi huo ulieleza kuwa tayari PBZ imeshafungua matawi matatu ya huduma za benki ya Kiislamu, na tawi la nne pamoja na Makao Makuu yake yatafunguliwa hivi karibuni katika jengo la ZIC.

Sambamba na hayo uongozi huo ulieleza juhudi ilizozichukua katika kuanzisha huduma za ATM, kuanzisha huduma za kibenki kwa njia ya simu za mkononi pamoja na internet, azma ya kutoa mikopo ya nyumba pamoja na kuanzisha huduma za kutuma fedha kwa wana Diaspora.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment