Tuesday, August 20, 2013

Dk.Shein apongeza PBZ

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesifu hatua zilizochukuliwa katika kuiimarisha Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) ikiwa ni pamoja na utoaji mikopo kwa wajasiriamali na kujiunga na mitandao mbali mbali kwa ajili ya kutoa huduma za kutuma fedha kwa wana Diaspora.

Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipokutana na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugrnzi wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), na kufanya nao mazungumzo huko Ikulu mjini Zanzibar.

Katika maelezo yake Dk. Shein alieleza kuwa mafanikio makubwa yameweza kupatikana kutokana na uongozi thabiti wa benki hiyo sambamba na umakini wa vionghozi wa Serikali kuu.

Alieleza matumaini yake makubwa katika benki hiyo kutokana na na hatua mbali mbali inazozichukua katika kujiimarisha hali ambayo itaimarisha uchumi na maendeleo ya Zanzibar na watu wake.

Kwa upande wa kujiunga na mitandao mbali mbali kwa ajili ya kutoa huduma za kutuma fedha kwa wana Diaspora, Dk. Shein alipongeza hatua hiyo na kusema kuwa italeta maendeleo makubwa na kuweza kutimiza azma ya serikali anayoiongoza.

Aliwataka wajumbe hao kutorudi nyuma na badala yake waendelee na juhudi zao hizo huku akieleza kuwa serikali imedhamiria kuwasaidia wajasiariamali na ndio maana ina mpango kabambe wa kuanzisha Mfuko maalum utakaowasaidia huku akipongeza azma ya PBZ ya kuwasaidia wajasiriamali.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza azma ya Serikali katika kuwasaidia wakulima kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa chakula na tayari imeshaanza kupunguza ruzuku pembejeo za kilimo zikiwemo matreka, dawa, mbegu, mbolea na kusisitiza mpango wa Serikali wa kununua matrekta 20 mwaka huu.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alipongeza juhudi za PBZ katika kuanzisha huduma za kibenki kwa njia ya mitandao ya simu za mkononi pamoja na internet, huduma ambayo itarahisiha upatikanaji wa huduma zake kwa urahisi zaidi.

Nao Wajumbe wa Bodi hiyo ya Wakurugenzi wa PBZ, walieleza maendeleo yaliopatikana na Benki hiyo baada ya uimarishaji wake na kueleza ukuaji wa amana za wateja na rasiliamli sambamba na ukuaji wa kikopo kwa wateja.

Bodi hiyo ilieleza kuwa PBZ imeweza jinsi ilivyofanyia matengenezo matawi yake ikiwa ni pamoja na kujenga jengo jipya la ChakeChake na kuweka mtandao wa ATM ili kupunguza foleni.

Aidha, Bodi hiyo ilieleza kuwa tayari imeshafungua matawi kutoka matawi matatu hadi matawi tisa na vituo vine katika sehemu mbali mbali, kuanzia mwaka 2010 hadi 2012.

Kwa upande wa huduma za benki ya Kiislamu uongozi huo ulieleza kuwa tayari PBZ imeshafungua matawi matatu ya huduma za benki ya Kiislamu, na tawi la nne pamoja na Makao Makuu yake yatafunguliwa hivi karibuni katika jengo la ZIC.

Sambamba na hayo uongozi huo ulieleza juhudi ilizozichukua katika kuanzisha huduma za ATM, kuanzisha huduma za kibenki kwa njia ya simu za mkononi pamoja na internet, azma ya kutoa mikopo ya nyumba pamoja na kuanzisha huduma za kutuma fedha kwa wana Diaspora.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.

Wanahaari pia wanajukumu la kutathimini kile wanachota kukifanyia kazi


Imeelezwa kuwa wanahabari kufanya kazi kwa uhakika na kutasmini kile ambacho anakitenda ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima. 

Tuesday, August 6, 2013

Dk.Sheni aungana na wananchi katika futari

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein jana aliungana na wananchi pamoja na viongozi mbali mbali wa Mkoa wa Mjini Magharibi katika futari maalum aliyowaandalia huko Ikulu mjini Zanzibar.

Akitoa shukurani kwa niaba ya Rais wa Zanzibar, Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein pamoja na wafanyakazi wa Ikulu, Waziri wa Nchi Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Mwinyihaji Makame alitoa shukurani hizo kwa wananchi kwa kuitikio mwaliko huo wa Rais.

Dk. Mwinyihaji Makame aliendelea kutoa shukurani hizo kwa wananchi kwa niaba kufuatia wananchi wengi kujitokeza katika futari hiyo maalum aliyoiandaa Rais.

Aidha, katika shukurani zake hizo Dk. Mwinyihaji Makame aliwapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kuendelea kuishi kwa upendo ikiwa ni pamoja na kudumisha amani, masikilizano na maelewano miongoni mwao.

Alisema kuwa hatua hiyo imepelekea wananchi kuweza kufanya ibada zao mbali mbali katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani kwa amani na utulivu mkubwa.

Pamoja na hayo, Dk. Mwinyihaji Makame alisisitiza kuwa umoja, mshikamano, upendo na masikilizano miongoni mwa wananchi wa Zanzibar ndio msingi mkubwa wa maendeleo huku akitoa shukurani kwa MwenyeziMungu kwa kuendelea kuijalia Zanzibar kuwa na mazao tofauti katika msimu huu wa kilimo.

Wananchi pamoja na Viongozi mbali mbali wa dini, vyama na Serikali walihudhuria akiwemo Makamo wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Rais Mstaafu wa Zanzibar Dk. Amani Abeid Karume, Waziri Kiongozi Mstaafu wa Zanzibar Ramadhani Haji Faki, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabih, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji, Mabalozi wadogo wa nchi za nje waliopo Zanzibar na wengineo.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.

Sunday, July 21, 2013

Dk.Shein afutarisha Pemba


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein jana ameungana na wananchi wa Mkoa wa Kusini Pemba katika futari maalum aliyowaandalia huko Ikulu ndogo ya Chake.

Akitoa shukurani kwa niaba ya Mhe. Rais Alhaj Dk. Shein, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mhe. Juma Kasim Tindwa alitoa shukurani kwa wananchi wote waliokubali mwaliko na kuhudhuria katika futari hiyo waliyoandaliwa na Rais ambayo imeonesha upendo mkubwa kwao.

Katika maelezo yake, Mkuu wa Mkoa huyo aliwasihi Masheikh katika Mkoa huo kuendelea kuhubiri amani na utulivu kwani hiyo ndio ngao pekee ya kujiletea maendeleo endelevu na kuishi katika maisha ya upendo.

Nao wananchi wa Mkoa wa Kusini Pemba wakitoa shukurani zao ambazo kwa niaba zilitolewa na Sheikh Mohammed Khamis na kueleza furaha za wananchi hao kwa kufutari pamoja na kiongozi wao wa nchi.

Katika maelezo yake Sheikh Khamis alitoa pongezi kwa Alhaj Dk. Shein kwa juhudi zake za kuwa karibu na wananchi katika shughuli mbali mbali za kimaendeleo zikiwemo za kidini.

Wananchi hao walieleza kuwa katika uongozi wa Rais Dk. Shein wameweza kuona uongozi wa uadilifu anaoufanya pamoja na kutumia busara kubwa na unyenyekevu katika kuongoza nchi.

“Tumeweza kuona uadilifu wako mkubwa katika kuongoza nchi ikiwa ni pamoja na kushiriki katika shughuli mbali mbali za kidini zikiwemo ufunguzi wa misikiti katika maeneo mbali mbali”,alisema Sheikh Mohammed Suleiman.

Pamoja na hayo, wananchi hao walimtakia uongozi mwema kiongozi huyo na kuiombea nchi iendelee kuwa na amani na utulivu na kuwasisitiza wananchi kuendelea kushirikiana pamoja.

Rajab Mkasaba, Pemba.

Tuesday, July 16, 2013

Dk.Shein atowa salama za rambi rambi kwa mkuu wa majeshi Tz

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, pamoja na wananchi wa Zanzibar wamepata mshtuko na huzuni kubwa kwa vifo vya wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi wa Watanzania walioshambuliwa na kuuawa wakati walipokuwa wakilinda amani katika eneo la Darfur, nchini Sudan.

Dk. Shein ameelezea kusikitishwa kwake na vifo hivyo na kueleza kuwa inasikitisha zaidi kuwa wanajeshi hao wamekufa wakiwa katika kazi ya kulinda amani nchini humo na kueleza kuwa wao ni mashujaa na wamekufa kishujaa.


Hayo yalielezwa katika salamu zake za rambi rambi alizotuma Dk. Shein kwa Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananachi wa Tanzania, Jenerali Davis Adolf Mwamunyange pamoja na wanajeshi wote, pia, salamu hizo zilitoa pole kwa familia za wafiwa.


Aidha, salamu hizo alizozituma Dk. Shein zilieleza kuwa huu ni msiba wa Taifa lote na wananchi wote wa Zanzibar wanaungana pamoja katika kuomboleza msiba huo.


“Tunatoa pole na tunamuomba MwenyeziMungu aziweke pahala pema peponi roho za mashujaa hao, vile vile tunawatakia nafuu ya haraka majeruhi wote wa tukio hilo”.


Alisisitiza Dk. Shein “ Mwenyezi Mungu akupeni moyo wa subira na ustahamilivu katika kipindi hiki cha msiba mkubwa”. zilieleza salamu hizo za rambirambi


Dk. Shein pamoja na wananchi wa Zanzibar wanaungana na Watanzania wenzao kuwaombea wale wote walioumia katika tukio hilo ili waweze kupona kwa haraka na kuendelea na majukumu yao ya ulinzi wa amani.


Vijana saba wa Jeshi la Wananachi wa Tanzania waliuawa baada ya kushambuliwa na waasi wa Sudan na wengine walijeruhiwa.


Wanajeshi hao wa Tanzania waliopoteza maisha yao pamoja na wale walioumia walikuwa ni sehemu ya askari 37 na ofisa mmoja ambao walikuwa wanasindikiza msafara wa waangalizi wa kijeshi katika eneo la Darfur.


Katika suala la ulinzi wa amani katika eneo hilo la Darfur, Wanajeshi kutoka Tanzania wamekuwa wakifanya kazi nzuri ya ulinzi tokea pale Tanzania ilipoanza kuchangia walinzi katika eneo hilo mnamo mwaka 2007, ambapo vijana hao waliouawa ni miongoni mwa vijana waliokwenda nchini humo Februari mwaka huu.


Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Dk.Shein aipongeza UNICEF

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amelipongeza Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia Watoto (UNICEF), kwa juhudi zake za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar.

Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Mwakilishi wa UNICEF nchini Tanzania Dk. Jama Gulaid, aliyefika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kumtambulisha Mama Francesca Moranditi atakayefanya kazi za Shirika hilo katika ofisi ya Zanzibar.


Katika maelezo yake Dk. Shein aliueleza uongozi huo wa UNICEF nchini Tanzaia kuwa Shirika hilo limekuwa na historia kubwa na mashirikiano na Zanzibar kwa muda mrefu.


Alieleza kuwa UNICEF imeweza kushirikiana vyema na Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo pamoja na huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na kuimarisha sekta ya afya, elimu pamoja na kuwasaidia na kuwajengea uwezo akina mama na watoto.


Dk. Shein katika maelezo yake alisema kuwa Shirika hilo limeweza kutoa msaada wake mkubwa kwa kushirikiana na Shirika la Afya duniani (WHO), katika kuimarisha sekta ya fya hapa nchini.


Alisisitiza kuwa Zanzibar imeweza kujiweka katika nafasi nzuri katika kufikia malengo ya Milenia katika sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya afya kwa kuweza kuungwa mkono na washirika wa maendeleo likiwemo shirika hilo la UNICEF.


“ Kwa upande wangu binafsi pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar tunatoa pongezi kwa UNICEF kwa kuendeleza ushirikiano wake kwetu na kuendelea kutuunga mkono kwa muda mrefu”,alisema Dk. Shein.


Aidha, Dk. Shein alisema kuwa kupungua vifo vya akina mama na watoto hapa nchini ni miongoni mwa mafanikio makubwa yaliopatikana na Setrikali ya Mapinduzi Zanzibar.


Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumkaribisha Mama Morandini hapa Zanzibar na kumuhakikishia kuwa mashirikiano makubwa atayapata kutoka kwa viongozi wa Serikali na wananchi wa Zanzibar kutokana na ukarimu wao na utamaduni wao wa kupenda wageni.


Mapema katika mazungumzo yake, Dk. Jama Gulaid alimueleza Dk. Shein kuwa Zanzibar imepata mafanikio makubwa katika kuimarisha sekta zake za maendeleo na kutoa pongezi zake kwa kuendelea kuwaenzi na kuwatunza watoto.


Alisema kuwa mbali na juhudi hizo Zanzibar imeweza kupata mafanikio katika kupunguza vifo vya akina mama na watoto pamoja na kupambana na Malaria hatua ambayo imeipa sifa Zanzibar ndani na nje ya Bara la Afrika.


Dk. Gulaid alieleza kuwa mabadiliko makubwa yameweza kutokea hapa nchini katika kuhakisha watoto wanapata haki zao za msingi pamoja na mahitaji yao muhimu juhudi ambazo zinaendelea kufanywa na Serikali anayoiongoza Dk. Shein.


Kutoka na juhudi hizo Mwakilishi huyo wa UNICEF nchini Tanzania alimuhakikishia Dk. Shein kuwa Shirika hilo litaendelea kutoa ushirikiano wake na kuendelea kuiunga mkono Zanzibar ili iweze kupata mafanikio zaidi.


Sambamba na hayo, Dk. Gulaid alimueleza Dk. Shein kuwa UNICEF itandelea kuwajengea uwezo wafanyakazi wake pamoja na kuziimarisha ofisi zake zote zilizopo hapa nchini Tanzania ili ziweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.


Nae Mama Francesca Morandini alitoa pongezi na shukurani kwa Dk. Shein kutokana na kumkaribisha Zanzibar na kumuahidi kuwa UNICEF inathamini na kutambua juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Shein hasa katika kuwajali watoto.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.

Wednesday, November 14, 2012

Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Dodoma



SMZ: Yasisitiza afya ya uzazi wa pango

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema kuwa jamii inahitaji kuelimishwa zaidi juu ya umuhimu wa uzazi wa mpango kwa maendeleo ya nchi na kutunza afya ya jamii hasa kwa akina mama na watoto.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad katika hafla ya uzinduzi wa Ripoti ya Idadi ya Watu Duniani ya mwaka 2012 iliyofanyika katika viwanja vya skuli ya Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambako alimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohd Shein.

Amesema jamii bado haijatoa umuhimu unaostahiki katika matumizi ya njia za uzazi wa mpango, hali inayopelekea kuwepo kwa ongezeko kubwa la watu ambalo huathiri harakati za maendeleo na afya ya jamii.

“Taarifa zinaonesha kwamba Zanzibar hivi sasa inakadiriwa kuwa na idadi ya watu 1.3 milioni, wanaoongezeka kwa kasi ya asilimia 3.1 kwa mwaka ambapo idadi ya watu katika kila kilomita moja ya mraba imefikia watu 496 mwaka 2011”, ilieleza sehemu ya hotuba hiyo ya Dkt. Shein iliyosomwa na Makamu wa Kwanza wa Rais.

Amefahamisha kuwa bado vifo vya mama wajawazito viko juu duniani lakini vimepungua kwa upande wa Tanzania na Zanzibar hasa kwa kina mama wenye umri mdogo na wanaokabiliwa na tatizo la umaskini.

“Kwa Tanzania katika mwaka 2004/05 idadi ya vifo ilikuwa 578 kwa kila akina mama waja wazito 100,000 na kupungua kidogo hadi kufikia vifo 454 mwaka 2010. Hata hivyo kwa Zanzibar vifo vya akina mama vimepungua kutoka vifo 473 mwaka 2006 hadi vifo 281 mwaka 2011, kwa kila kina mama 100,000 kwa takwimu za hospitali”, alifafanua.

Amesema mafanikio hayo yametokana na juhudi za serikali katika kuimarisha huduma za afya kwa jamii ikiwa ni pamoja na kutoa chanjo za pepopunda na shurua, sambamba na kuimarisha huduma za afya ya uzazi katika hospitali mbali mbali.

Kwa upande wao wawakilishi wa Umoja wa Mataifa wameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuona umuhimu wa huduma ya uzazi na kuamua kutoa huduma hiyo bila ya malipo.

Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Idadi ya watu (UNFPA) Tanzania bibi Mariam Khan amesema bado suala la uzazi wa mpango linakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na wanajamii kuona ugumu juu ya matumizi ya njia za uzazi wa mpango.

Amefahamisha kuwa uzazi wa mpango ni muhimu katika kusaidia kukuza kipato cha wanafamilia, sambamba na kuwaendeleza watoto katika makuzi bora, na wito kwa jamii kutoa fursa zinazostahiki kwa akina mama na watoto ili kusaidia harakati za maendeleo kwa jamii.

Waziri wa Afya Mhe. Juma Duni Haji amesema wameamua kufanya uzinduzi huo katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, ili kutoa uelewa zaidi kwa wakaazi wa Mkoa huo ambao ni miongoni mwa mikoa inayofanya vibaya katika suala la uzazi wa mpango.

Amesema akinamama na watoto wanahitaji kulindwa kiafya, na kuwataka wazazi kushirikiana katika suala la malezi na makuzi ya watoto.

Mapema akitoa muhtasari wa ripoti hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Khamis Mussa amesema kimsingi ripoti hiyo imeelezea juu ya changamoto, faida na haki za binadamu katika uzazi wa mpango.

Amesema uzazi wa mpango ni miongoni kwa haki za binadamu lakini imeelekezwa zaidi kwenye haki za kifamilia, ili wanafamilia waweze kupanga juu ya idadi na umri wa kupishana kwa watoto, ili kuepuka mimba zisizotarajiwa.

“Inakisiwa kuwa kiasi cha mimba milioni 80 zinapatikana bila ya kutarajiwa duniani, huku nusu ya mimba hizo zikitolewa, jambo ambalo ni hatari nyengine katika uzazi”. Alidokeza Katibu Mkuu huyo.

Hassan Hamad, OMKR.

Friday, November 9, 2012

Dr.Shein ampongeza Obama

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein ametuma salamu za pongezi kufuatia ushindi wa Rais Barack Obama wa Marekani katika Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo uliofanyika hivi karibuni.
 
Katika salamu zake za pongezi kwa kiongozi huyo wa Marekani ambaye amechaguliwa kwa mara nyengine tena na wananchi wa nchi hiyo kwa kipindi cha pili, Rais Dk. Shein alieleza jinsi alivyopokea kwa furaha ushindi huo pamoja na wananchi wote wa Zanzibar.
 
Salamu hizo za pongezi zilieleza kuwa kwa niaba yake binafsi pamoja na wananchi wa Zanzibar anatuma salamu za pongezi kwa Rais Obama kwa ushindi mkubwa alioupata katika uchaguzi uliofanyika hivi karibuni nchini humo.
 
Aidha, salamu hizo zilieleza kuwa  wananchi wa Marekani wameona umuhimu wa kumuunga mkono Rais Obama na kumrejesha tena madarakani kwa lengo la kuliendeleza na kuliongoza taifa hilo kubwa duniani kwa kipindi cha miaka mine ijayo.
 
Pamoja na hayo, salamu hizo zilieleza kuwa wananchi wa Zanzibar wanaungana na rafiki zao wa Marekani katika kusherehekea ushindi huo uliotokana na uchaguzi mkuu wa hivi karibuni wa Marekani ambao umempa ushindi Rais Obama.
 
Dk. Shein alimtakia uongozi mwema Rais Obama na kutoa salamu za pongezi kwa familia ya Rais Obama akiwemo Mkewe Mama Michelle Obama  na watoto wake wote Malia na Sasha Obama  pamoja na wananchi  wa Marekani ambao wameonesha wazi imani na uaminifu mkubwa walionao katika uongozi wa Rais Obama.
 
Sambamba na hayo, salamu hizo zilieleza kuwa  uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Zanzibar na Marekani utazidi kuimarika.
 
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.

Balozi wa India akutana na Dr.Shein Ikulu Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameleza haja kwa Serikali ya India kurejesha utamaduni uliokuwa ukifanya miaka ya nyuma wa kuwaleta madaktari bigwa kwa amu hapa Zanzibar hatua ambayo ilisadia sana kuimarisha sekta ya afya na kutoa huduma kwa jamii wakati huo.

Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Balozi mdogo wa India aliopo Zanzibar Mhe. Pawan Kumar ambaye alifika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha.


Dk. Shein alisema kuwa mnamo miaka ya 1970 hadi mwanzoni mwa miaka ya 1980, India ilikuwa na utaratibu huo wa kutela madaktari bingwa hapa Zanzibar ambao waliweza kufanya kazi zao na kutoa huduma za afya kwa wananchi hatua ambayo ni busara kuanzishwa tena ili kuendeleza kuimarisha sekta ya afya hapa Zanzibar.


Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa kuwepo kwa madaktari bigwa hapa nchini kutoka India kutasaida zaidi kuimarisha huduma katika hospitali za Zanzibar hasa hospitali za Wete na Chake kisiwani Pemba ambazo kwa hivi sasa zina upungufu wa madaktari bigwa.


Mbali na hatua hiyo, Dk. Shein alisisitiza umuhimu wa kubadilishana uzoefu na utaalamu kwa madatari wa India na Zanzibar kwa awamu, juhudi ambazo zitasaidia kuipinguzia gharama Serikali ya kupelekea wagonjwa katika hospitali zilizopo nchini humo.
 
Aidha, Dk. Shein alieleza haja ya kuanzisha Mkataba wa Makubaliano juu ya kuimarisha sekta ya afya kati ya India na Zanzibar.

Pia Dk. Shein alimueleza Balozi huyo uhusiano wa siku nyingi katika sanaa ya uimbaji ambao upo kati ya India na Zanzibar hali ambayo ilimpelekea mwimbaji maarufu marehemu Siti Binti Saad kwenda kurikodi katika studio za nchi hiyo nyimbo zake mbali mbali ambazo zilimjengea sifa kubwa duniani.


Kwa upande wa sekta ya kilimo, Dk. Shein alieleza kuwa kutokana na India na Zanzibar kufanana kijiografia kuna umuhimu wa nchi hizo kuendeleza ushirikiano katika sekta hiyo ambayo ni tegemeo kubwa la uchumi wa Zanzibar na wananchi wenyewe.


Dk. Shein alieleza kuwa India ni miongoni mwa nchi zilizopiga hatua katika kufanya utafiti wa kilimo hivyo alieleza haja ya kuimarisha ushirikiano katika sekta hiyo hasa kwa kushirikiana na wataalamu wa Kitengo cha Utafiti wa Kilimo kiliopo Kizimbani.


Kutokana na Balozi huyo kuwa mpya katika mazingira ya Zanzibar Dk. Shein alimshauri kutembelea katika maeneo ya kilimo cha mpunga ili aweze kuona uhalisia na hatua zilizofikiwa na wananchi pamoja na juhudi za serikali za uimarishaji wa sekta hiyo.


Akieleza juu ya zao la karafuu, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa kwa vile India wana historia ya ununuzi na utumiaji wa karafuu kutoka Zanzibar hivyo ipo haja kya kuimarisha ushirikiano wa kibiashara katika zao hilo.


Pia, Dk. Shein alipongeza maendeleo makubwa yaliofikiwa na India katika sekta ya elimu na kueleza kuwa nchi hiyo hivi sasa imekuwa ikitoa mafunzo mbali mbali kwa wanafunzi kutoka nchi tofauti duniani na kueleza kufarajika kwake kutokana na wanafunzi wengi wanaotoka Zanzibar na kwenda nchini humo kusoma fani mbali mbali.


Sambamba na hayo, Dk. Shein alisisitiza haja ya kuendeleza ushirikiano katika sekta hiyo ya elimu huku akipongeza juhudi za India za kutaka kuanzisha Chuo cha Mafunzo ya Amali huko kisiwani Pemba pamoja na juhudi za kuanzisha mradi wa kutoa mafunzo kwa watoto wa kike vijijini.


Nae Balozi huyo mdogo wa India aliopo hapa Zanzibar Mhe. Pawan Kumar alimueleza Dk. Shein kuwa nchi yake itaendeleza uhusiano na ushirikiano uliopo ambao ni wa muda mrefu na umekuwa na historia kubwa.


Balozi Pawan Kumar alieleza kupokea rai zilizotolewa na Dk. Shein katika kuimarisha sekta ya afya nchini pamoja kuahidi kuzifanyia kazi ipasavyo.


Alieleza kuwa kwa upande wa sekta ya Afya India itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa nafasi za masomo kwa madaktari wazalendo. Aidha, Balozi huyo alieleza kuwa mbali ya nafasi za masomo kwa madaktari wazalendo pia, nchi hiyo itaendelea kutoa nafasi za masomo katika fani nyengine tofauti.
 

Balozi Pawan Kumar pia, alibainisha kuendeleza ushirikiano katika kuimarisha nishati pamoja na juhudi za kujikinga na maafa.

Pamoja na hayo, Balozi huyo alimueleza Dk. Shein azma ya India ya kujenga Chuo cha Amali kisiwani Pemba, hatua ambayo itasaidia katika kuimarisha sekta ya ajira na kutoa utaalamu kwa wananchi.
 

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.

Wednesday, October 17, 2012

Dk.Shein awaapisha viongozi wapya

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein leo amewaapisha viongozi na watendaji katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kufuatia uteuzi alioufanya hivi karibuni.
 
Katika hafla hiyo iliyofanyika Ikulu mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali Dk. Shein alimuapisha Mhe. Shawana Bukheti Hassan ambaye ameapishwa kuwa  Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na Waziri asiekuwa na Wizara Maalum.
 
Miongoni mwa viongozi waliohudhuria ni Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Balozi Seif Ali Idd, Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Pandu Ameir Kificho, Waziri wa Nchi Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Mwinyihaji Makame
 
Wengine ni Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Mohammed Aboud, Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Mhe. Ramadhan Abdalla Shaaban, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdillahi Jihad Hassan, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mhe. Abdalla Mwinyi Khamis, Meya wa Manispaa ya Mji wa Zanzibar, Mstahiki Khatib Abdulrahman Khatib pamoja na viongozi wengine.
 
Wakati huo huo, Dk. Shein amewaapisha viongozi wengine akiwemo Naibu Waziri wa Kilimo na Maliasili Mhe. Mtumwa Kheir Mbarak pamoja na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mohamed Said Mohamed.
 
Viongozi wengine walioapishwa katika hafla hiyo ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Bwana Tahir M. Abdalla pamoja na Bwana Mustafa Aboud Jumbe ambaye ambae ameapishwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano.
 
Pia, Dk. Shein amemuapisha Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi anaeshughulikia Idara Maalum za SMZ, CDR Julius Nalimy Maziku pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais (Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo) Bwana Juma Ameir Hafidh.
 
Hapo juzi, Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein alifanya mabadiliko ya viongozi na watendaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kutumia uwezo aliopewa chini ya vifungu vya  Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ambapo pia, alifuta rasmi uteuzi wa Mhe. Mansoor Yussuf Himid kuwa Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi kuanzia Oktoba 15 mwaka huu na Mhe. Shawana Bukheti Hassan aliteuliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi.
Rajab Mkasaba, Ikulu

Tuesday, September 11, 2012

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


KUUAWA KWA MWENYEKITI WA KLABU YA WAANDISHI WA HABARI MKOA WA IRINGA (IPC) DAUDI MWANGOSI 
 Zanzibar Press Club imepokea kwa masikitiko na hudhuni  taarifa ya kifo cha mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten ambaye pia ni Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari wa Iringa.  
Zanzibar Press Club inaungana na waandishi wa habari wote nchini ambao leo hii wanatekeleza azimio la jukwaa la Wahariri la kufanya maandamo ya kimya kimya, kote nchini, kwa lengo la kupinga mauwaji ya aliyekuwa Mwenyekiti Klabu ya waandishi wa habari wa Iringa, Mrehemu Daudi Mwangosi.
Katika kutekeleza azimio hilo ZPC imeamuwa kukutana na waandishi wa habari ili kuweza kueleza kusikitishwa kwao na tukio hilo lilompata mwenzetu wakati akitekeleza majukumu yake ya kila siku.
Aidha ZPC inaungana na waandishi na wafanyakazi katika tasnia ya habari nchini, Umoja wa Waandishi wa Habari nchini (UTPC), Klabu za waandishi kote nchini, MISA-TAN, MCT, JUKWAA LA WAHARIRI  n.k  pamoja na familia ya marehemu Daudi Mwangosi kwenye kipindi  hiki kigumu cha msiba, ambapo hakuna shaka kwamba tasnia ya habari nchini imelazimika kuingia matatani kutokana na matumizi mabaya ya nguvu na  mabavu ya Jeshi la Polisi.
ZPC inalaani kwa nguvu zote mauwaji hayo na yaliyofanywa na watendaji wa taasisi ya umma pamoja na kutumia nguvu nyingi kupiti kiasi zilizopelekea kifo cha mwandishi huyo.
Jeshi la Polisi limekuwa likiendeleza tabia yake ya  matumizi ya nguvu kupita kiasi kwa raia wa taifa hili. Ipo haya ya kutaka kujuwa ni hadi lini jeshi la polisi wataweza kuimarisha vyema shughuli za ulinzi bila ya kuchukuwa uhai wa mtu?
Hapana shaka yoyote kwamba kifo cha Daudi Mwangosi kimegubikwa na utata wa kutosha kuanzi mwazo hadi mwisho wa maisha yake, na hasa ukizingatia kwamba tukio hilo la mauaji limefanyika hadharani wakati  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa Nd.Michael Kamuhanda alikuwa anatambua uwepo wa Daud Mwangosi  na pia umuhimu wa habari hizo kwa taifa, na kibaya zaidi ni pale kumuona Daud akiwa anafia kwenye mikono ya jeshi la polisi kulikoni?
Ikumbukwe kwamba siku zote hata katika vita waandishi wanafanya kazi bega kwa bega na askari ili kuwajuza wananchi nini kinachotokea na kinachoendelea kwenye uwanja wa mapambano.
Kutoka na kifo hicho ZPC inaomba hatua za kisheria zichukuliwe kwa wale wote waliohusika moja kwa moja na kifo cha mwandishi huyo.
Zanzibar Press Club kwa saa ingependa kuona utekelezaji mzuri wa kisheria kwa askari wote ambao walihusika kwenye kadhia hii.
Mbali na hayo, ZPC inawaomba waandishi wa habari wote wa Zanzibar wawe makini wakati wanapotekeleza majukumu yao, kwani kutokana na tukio hili limetufanya tuone kuwa Jeshi la Polisi ni Mdau anayetutia shaka katika utekelezaji wa majukumu yetu.
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi Amini.
Abdalla Juma Pandu
Kaimu Mwenyekiti
Zanzibar Press Club

Wednesday, June 13, 2012

SMZ ipo pamoja na wananchi wake

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katu hawatowasaliti wananchi wa Zanzibar katika kutoa maoni ya uundwaji wa katiba mpya ya Tanzania. 
Amesema viongozi wataheshimu na kutetea maoni ya wananchi wanatakayoyatoa kwenye Tume ya marekebisho ya katiba, na kutoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kutoa  maoni yao wakati utakapofika.
Maalim Seif ametoa kauli hiyo leo huko Eacrotanal Mjini Zanzibar alipokuwa akizindua kongamano linalohusu Muungano na Mchakato wa mabadiliko ya katiba ya Tanzania lililoandaliwa na kituo cha huduma za sheria Zanzibar.
Amesema kila mtanzania atakuwa huru kutoa maoni yake, na kwamba  ni fursa muhimu kwa Wazanzibari kueleza kero zinazowakabili ndani ya Muungano, badala ya kukaa kimya na kusubiri maamuzi yasiyokuwa na mustakbali mzuri na nchi yao.
Makamu wa Kwanza wa Rais amekiri kuwepo kwa kero nyingi za Muungano ambazo zinahitaji kutatuliwa kwa haraka ili kupunguza malalamiko ya wananchi wa pande mbili za Muungano.
Amefafanua kuwa kwa sasa yapo mawazo mengi kuhusu muundo wa Muungano, lakini amesema ni vyema kila nchi kati ya Tanganyika na Zanzibar ikawa na mamlaka yake kamili, kisha uanzishwe Muungano wa mkataba kwa mambo ambayo nchi mbili hizi zitakubaliana.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kituo cha huduma za sheria Zanzibar Profesa Chris Maina Peter amesema ni muhimu kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika kuunda katiba yao, ikizingatiwa kuwa katiba zilizopita hazikuwashirikisha wananchi moja kwa moja.
Nae Mwakilishi wa Shirika la Ford Foundation kanda ya Afrika Mashariki bwana Maurice Makoloo amesema shirika lake ambalo limekuwa likisaidia miradi mbali mbali ikiwemo kukuza demokrasia na kupunguza umaskini, litaendelea kushirikiana na Tanzania katika mchakato wake wa mabadiliko ya katiba ili kutimiza lengo lake la kukuza demokrasia katika nchi za Afrika Mashariki.
  Hassan Hamad (OMKR).

Tuesday, June 12, 2012

Tume ya taifa ya sayanzi yaombwa kuwahsjihisha wasomi

Uongozi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia Tanzania {costech} umeombwa kushajiisha Wasomi hasa Vijana wa Vyuo Vikuu Nchini kupenda kufanya tafiti mbali mbali zitakazojenga Mazingira ya kumuondoa  Mtanzania kwenye matatizo yanayomkabili.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa ombi hilo katika Hafla fupi ya uzinduzi wa Ofisi ya Tume hiyo ilyofanyika hapo Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja.
Balozi Seif alisema Tafiti kama hizo ambazo zitakuwa na uhusiano wa moja kwa moja na Mwananchi  zinaweza kusaidia kupata Maendeleo kwa kasi zaidi katika Kipindi kifupi kijacho.
Alisisitiza kwamba Serikali kwa upande wake iko tayari kwa namna yoyote ile kutumia vyema matokeo ya Tafiti zinazofanywa na Wazomi wazalendo.
Hata hivyo Balozi Seif alieleza kuwa yapo baadhi ya matokeo ya Tafiti hubakia kuwa siri kwa Taifa lakini mengine yanastahiki kutolewa kwa Wananchi ili waelewe kinachoendelea kwenye maisha yao.
Balozi Seif alieleza kwamba wakati umefika kwa Makampuni pamoja na Viwanda vya hapa Nchini kujenga Utamaduni wa kutoa kazi zao za Utafiti kwa Tume hiyo ili ijipatie fedha za kuendesha shughuli zake za utafiti kama Nchi nyengine zilizoendelea.
Alieleza kwamba Tanzania imepania kuleta maendeleo kwa Wananchi wake kutokana na uamuzi wake wa kutenga Jumla ya shilingi za Kitanzania Bilioni Thalathini { 30,000,000,000/-} kwa ajili ya Utafiti na Maendeleo kwenye Bajeti yake ya Mwaka 2010/2012.
Balozi Seif alifahamisha kwamba Maendeleo bila ya Sayansi na Teknolojia  hayapatikani kwani masuala hayo mawili yanakaribiana katika utekelezaji wake.
Akizungumzia Tume ya Taifa ya nguvu za Atomu Balozi Seif  alielezea kufarajika kwake kutokana na mipango m,izuri ya Taasisi hiyo kuhudumia Zanzibar katika masuala ya usimamizi wa matumizi salama  ya Mionzi.
Balozi Seif alisema ushirikiano wa pamoja wa Taasisi hiyo,Wizara ya Afya Zanzibar na Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani katika kuanzisha  mradi wa Matibabu ya Saratani katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja unafaa kuungwa mkono.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameishukuru Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uamuzi wake wa  wa kusogeza karibu na Wananchi shughuli za  Ofisi ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Tume ya Taifa ya  Nguvu za Atomu.
Katika Taarifa yake Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania Profesa Iddi Suleiman Nyangarika Mkilaha alisema Taasisi yake itaendelea kutoa Elimu sahihi ya matumizi ya Mionzi.
Profesa Nyangarika alisema Taaluma hizo kwa sasa itazingatia zaidi katika sekta ya Viwanda pamoja na Vituo vya Afya ambavyo vinatumia Vifaa vyenye mazingira ya Nguvu za Atomiki.
Mkurugenzi huyo wa Tume ya Nguvu za Atomiki alifahamisha kwamba katika kupanua zaidi huduma zake Taasisi hiyo itaendelea kupima Mionzi katika Mimea ili kujua kiwango sahihi cha kulinda Vyakula kwa ajili yamatumizi bora kwa Wanaadamu.
Mapema Waziri wa Mawasiliano,Sayansina Teknolojia wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Makame Mnyaa Mbarawa alisema Wizara hiyo itaendelea kushirikiana na Wataalamu wa ndani na nje ili kuona Tafiti zinazofanywa zinatmika kwa walengwa ambao ni Wananchi.
Alisema Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia na ile ya Nguvu za Atomiki zimeanzishwa zikiwa na wajibu wa kusimamia tafiti na nguvu za Atomiki Nchini kwa kushirikiana na Taasisi za Kanda na zile za Kimataifa.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Mkamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Friday, June 8, 2012

Msumbiji yakumbusha ufugaji wa samaki Zanzibar

Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa Msumbiji imekumbushwa tena kufikiria ombi la Zanzibar la kuipatiwa Wataalamu katika kuendeleza Sekta ya ufugaji wa Samaki wa Kamba.
Ombi hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati wa mazungumzo yake na Balozi wa Msumbiji Nchini Tanzania Bwana Zakaria Kupela yaliyofanyika hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Msumbiji imekuwa na uzoefu wa muda mrefu katika shughuli za ufugaji wa kamba  na kujipatia umaarufu sehemu mbali mbali Duniani.
Alisema utaalamu na uzoefu ulioipata Nchi hiyo unaweza kuisadia Zanzibar katika moja ya harakati zake za kujenga mazingira ya ajira kwa Vijana wake.
“ Sio mbaya kukukumbusha tena lile wazo letu nililokuelezea  wakati ule tulipokutana kwa mara ya kwanza ingawa inaonekana kulikuwepo na tatizo la ufuatiliaji wa suala hilo”. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza Balozi Mdogo wa Msumbiji Bw. Zakaria Kupela kwa juhudi zake za kuendelea kuunganisha uhusiano uliopo kati ya Msumbiji na Tanzania na Zanzibar kwa Ujumla.
Balozi Seif alifahamisha kwamba uhusiano wa pande hizo mbili ni wa maumbile kutokana na maingiliano ya kidamu yaliyopo kati ya Wananchi wa Tanzania na Msumbiji.
Mapema wa Msumbiji aliyemaliza muda wake hapa Tanzania Bwana Zakaria Kupela alishauri rasilmali zilizopo kwa Mataifa yote mawili ni vyema zikawekewa mikataba kwa faida ya Vizazi vijavyo.
Balozi Kupela alisema Mataifa yote mawili yamebarikiwa kuwa na rasilmali nyingi mfano Maji,Madini, Gesi na Bahari ambazo kama hazikuwekewa utaratibu wa matumizi mazuri zinaweza kuchukuliwa na wajanja.
Alifahamisha kwamba Kizazi kijacho kinaweza kukumbwa  na ushawishi wa Baadhi ya Mataifa au mashirika ya Nje katika matumizi ya rasilmali hizo kinyume na  haki ya Mataifa husika.
Alisisitiza suala la kuendelezwa utaratibu wa kubadilishana Wanafunzi kati ya Tanzania na Msumbiji ambao utasaidia zaidi uhusiano wa pande hizo.
Balozi Kupela ameelezea faraja yake kuona nyanja hiyo imeshaleta matunda kwa vile tayari yapo mabadilishano ya wanafunzi 50 wa mwaka wa pili sasa kati ya Tanzania na Msumbiji.
Alisema mpango huo ukiandaliwa vyema unaweza pia kuratibu mafunzo yatakayowawezesha Vijana wa pande zote mbili hizo kuelewa vyema kizazi kilicholeta ukombozi kwa Mataifa hayo mawili.
Kuhusu suala la Amani Balozi Kupela aliwanasihi Wananchi wa Zanzibar kuendeleza amani waliyonayo ndani ya mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa  ambayo hivi sasa ni darasa kwa mataifa mengine Duniani.
Balozi Kupela alitahadharisha kwamba kitu chochote chenye cheche ya kutenganisha jamii ni hatari kwa faifa ya kizazi kijacho.
Balozi Kupela alifika Ofisini kwa Balozi Seif kuaga rasmi na kurejea Nyumbani Msumbiji baaada ya kumaliza muda wake wa Utumishi hapa Tanzania.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Wednesday, June 6, 2012

Mbaraka Juma Ali anatafutwa kwa kosa la wizi


   Mnamo tarehe 20 may 2012 siku ya jumapili ulifanyika wizi wa mali za ofisi ya zanzibar press club na mali za IS-HAKA OMAR RWEYEMAMU kwa mujibu wa polisi zinakadiliwa kuwa na thamani ya TSH.11,600,000 uliofanywa na kijana anayeitwa Mbaraka Juma Ali mkaazi wa zanzibar,wizi huo ulifanyika katika mtaa wa michenzani block no.7 ghorofa ya tatu mali zilizoibiwa ni pamoja na
                                   1.Radio aina ya panasonic
                                   2.kompyuta aina laptop
                                   3.sanduku   la nguo
                                   4.passport ya kusafiria
                                   5.dvd player.
                                   6.cheti cha kuzaliwa