Tuesday, August 6, 2013

Dk.Sheni aungana na wananchi katika futari

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein jana aliungana na wananchi pamoja na viongozi mbali mbali wa Mkoa wa Mjini Magharibi katika futari maalum aliyowaandalia huko Ikulu mjini Zanzibar.

Akitoa shukurani kwa niaba ya Rais wa Zanzibar, Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein pamoja na wafanyakazi wa Ikulu, Waziri wa Nchi Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Mwinyihaji Makame alitoa shukurani hizo kwa wananchi kwa kuitikio mwaliko huo wa Rais.

Dk. Mwinyihaji Makame aliendelea kutoa shukurani hizo kwa wananchi kwa niaba kufuatia wananchi wengi kujitokeza katika futari hiyo maalum aliyoiandaa Rais.

Aidha, katika shukurani zake hizo Dk. Mwinyihaji Makame aliwapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kuendelea kuishi kwa upendo ikiwa ni pamoja na kudumisha amani, masikilizano na maelewano miongoni mwao.

Alisema kuwa hatua hiyo imepelekea wananchi kuweza kufanya ibada zao mbali mbali katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani kwa amani na utulivu mkubwa.

Pamoja na hayo, Dk. Mwinyihaji Makame alisisitiza kuwa umoja, mshikamano, upendo na masikilizano miongoni mwa wananchi wa Zanzibar ndio msingi mkubwa wa maendeleo huku akitoa shukurani kwa MwenyeziMungu kwa kuendelea kuijalia Zanzibar kuwa na mazao tofauti katika msimu huu wa kilimo.

Wananchi pamoja na Viongozi mbali mbali wa dini, vyama na Serikali walihudhuria akiwemo Makamo wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Rais Mstaafu wa Zanzibar Dk. Amani Abeid Karume, Waziri Kiongozi Mstaafu wa Zanzibar Ramadhani Haji Faki, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabih, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji, Mabalozi wadogo wa nchi za nje waliopo Zanzibar na wengineo.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment