Wednesday, February 22, 2012

Maalim Seif awataka watendaji wa chama cha CUF kuwa karibu na wanachama wao

Na Is-haka Omar ZPC Zanzibar
Katibu mkuu wa chama cha wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad amewataka watendaji wa chama hicho ngazi ya wilaya kufanya kazi kwa karibu na wanachama ikiwa ni hatua muhimu katika kukijenga chama chao.
Amesema watendaji hao wana nafasi kubwa katika kukijenga na kukiimarisha chama hicho, ikizingatiwa kuwa wao ndio wenye mawasilianao ya karibu zaidi na wanachama pamoja na wananchi kwa ujumla.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ametoa wito huo leo katika hoteli ya mazsons shangani mjini zanzibar, wakati akifungua semina elekezi kwa wenyeviti na makatibu wa wilaya wa chama cha CUF, yenye lengo la kujadili dhana ya utumishi wa umma.
Amewataka wajumbe wa mkutano huo kuijadili dhana hiyo kwa umakini mkubwa, kwa kuzingatia zaidi maslahi na maendeleo ya chama hicho, sambamba na kuhimiza suala la uwajibikaji kwa viongozi wa ngazi zote za chama.
Semina hiyo imehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa chama hicho wakiwemo wenyeviti na makatibu wa wilaya kutoka wilaya zote za unguja na Pemba.

No comments:

Post a Comment