Friday, February 24, 2012

Miti elfu moja yatarajiwa kupandwa ikiwa ni miongoni za njia bora za kuhifadhi misitu Zanzibar

Na Is-haka Omar ZPC
Kiasi ya miti elfu moja inatarajiwa kupandwa katika sehemu za wazi za kijiji cha Jendele hadi Cheju ikiwa ni harakati za kuimarisha hifadhi ya misitu na utunzaji wa mazingira katika vijiji hivyo.
Mradi huo unatarajiwa kutekelezwa na kamati ya uhifadhi wa misitu ya asili ya cheju pembezoni mwa barabara ambapo hivi sasa wanasubiri utekelezaji wa ujenzi wa barabara inayounganisha vijiji hivyo uanze ili kuona maeneo muafaka yatakayotumika.
Sheha wa shehia ya cheju Bw.Kassim Suleiman Mdunga amesema wameshatoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa idara ya mistu ili kupatiwa msaada na maelekezo zaidi juu ya zoezi hilo.
Amefahamisha kuwa shehia hiyo imeamua kupanda miti ya miembe boribo ambayo ni miongoni mwa mimea inayoanza kupotea kutokana na ongezeko la watu kujihusisha na shughuli za ukataji miti kwa ajili ya kujiongezea kipato na matumizi ya kijamii.
Kwa upande wake sheha wa shehia ya jendele Bw.Ame Makame Rajab ameiomba serikali kuhamasisha jamii katika kutafuta mbinu mbadala zitakazosaidia kupumguza vitendo vya ukataji miti kiholela katika shehia hizo.

No comments:

Post a Comment