Wednesday, February 29, 2012

WATU WENYE KUISHI NA ULEMAVU

Na Is-haka Omar ZPC
Kwa miaka mingi sasa ,suala la ulemavu halikuwa na umuhimu wowote katika jamii kutokana na mitizamo na imani potofu ingawa ulemavu umekuwa ukiongezeka siku hadi siku kutokana na sababu za kiuchumi,kisiasa ma kijamii.
Suala hili limeanza kuzungumzwa baada ya mwaka wa kimataifa wa watu wenye ulemavu (1981)ambapo umoja wa mataifa na jumuiya za watu wenye ulemavu dumiani zilipoanza kutetea ulemavu kama suala la haki ya binadamu.
Katika takwimu za kimataifa zinabainisha kuwa zaidi ya watu bilioni 1.5 wanapata ulemavu kila mwaka kupitia vyanzo mbalimbali vya kimaisha, lakini idadi hiyo inashamiri zaidi katika nchi zenye migogoro ya kivita kwani nchi hizo zinakuwa na watu wengi wenye ulemavu.
Tunatakiwa kufahamu maana ya ulemavu pamoja na kutofautisha aina hizo na viwango vya ulemavu,na kuelewa sababu za mtu kupata ulemavu katika kuelimisha jamii jinsi ya kujikinga na ulemavu sambamba na kuelewa changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu kidunia.
Tukumbuke kuwa ulemavu ni athari ya muda mfupi au ya kudumu inayosababishwa na hitilafu za kiwiliwili au hisia mfano uoni,usikivu,akili,kusema na kumsababishia mtu kushindwa kufanya kazi kikawaida.
Katika uchambuzi wa makala hii umebainisha aina kuu za ulemavu kuwa ni pamona ulemavu wa viungo,ulemavu wa uoni,kiziwi na matatizo ya kusema,ulemavu wa akili,albino (ulemavu wa ngozi) mwingineo kama kifafa,kichwa kikubwa mpasuko wa mdomo pamoja na ulemavu mchanganyiko ambapo mtu anakuwa na ulemavu zaidi ya mmoja.
Pia ulemavu umegawanyika katika viwango tofauti kuna ulemavu mdogo huu mtu anakuwa hitilafu au kasoro ndogo katika mwili au hisia lakini anaweza kujihudumia na kufanya kazi zote,lakini upo ulemavu wa kiasi mtu anaweza kujihudumia na kufanya kazi endapo atatumia visaidizi na mazingira yanapoboreshwa katika kiwango cha ulemavu mkubwa mtu huitaji kusaidiwa katika maisha yake yote.
Zipo sababu nyingi mtu ambazo anaweza kupata ulemavu kama kurithi,vita,utumiaji ovyo wa dawa za kulevya,magonjwa kama shinikizo la damu,kisukari,homa kali,surua,ajali,kupigwa,huduma duni kwa mama wajawazito wakati wa kujifungua na kupata mimba kwenye umri wa chini ya miaka 18 au zaidi ya miaka 35.
Changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu hapa nchini ni pamoja na kubaguliwa kijamii,kisiasa na kiuchumi mambo ambayo yakuwa vikwazo juu ya maisha yao ya kila siku na kusababisha wao kujiona kama watu ambao hawana umuhimu au haki ya kuishi kama watu wengine.
Ukosefu wa haki za msingi kama elimu,ajira na tiba zinazohusiana na wao pia ni tatizo ambalo linakua kwa kasi kubwa katika jamii yetu, licha ya kutolewa kwa elimu tofauti juu ya haki na usawa kwa watu wenye ulemavu juhudi za serikali pamoja na asasi binafsi katika kuhamasisha jamii kuondokana na dhana mbaya juu ya watu hawa ambayo wengi wanaamini kuwa watu wenye ulemavu ni moja ya jamii ambayo inahitaji msaada wa kila mara jambo ambalo si sahihi bali wanahitaji kuandaliwa mazingira mazuri ya kuweza kujitegemea wenyewe au kupewa msaada wa kielimu kama ujasilia mali ili waweze kujikimu kimaisha bila ya kutegema msaada wa mtu au taasisi fulani.
Umbali wa huduma za msingi unachangia katika kukwamisha maendeleo ya watu wenye ulemavu kwani ushindwa kufikia huduma muhimu kwa kukosa usafiri unaoendana na mazingira halisi ya watu hao,hivyo kama ni wanafunzi ushindwa kufika katika skuli au vyuo kwa muda unaotakiwa hata sehemu zao za kutafuta riziki yaani kazi halali ambayo ni haki ya msingi kwa kila mtu ,kufikia sehemu hizo upata vikwazo katika usafiri ikiwa katika daladala na aina zingine za usafiri.
Katika suala zima la kiuchumi wengi wao hukosa vyazo vya kujiingizia kipato yaani fedha na kujikuta wanashindwa kupata huduma za msingi au kushindwa kufanya biashara kutokana na hitilafu za kimaumbile walizonazo,hivyo upelekea kutomudu gharama za kununulia visaidizi vya kuwasaidia katika maisha yao ya kila siku.
Mazingira yasiyofikika nayo ni kikwazo kikubwa kwa watu hawa kwani wanashindwa kufikia huduma muhimu za kibinadamu hususani sehemu za majengo ya kwenda juu yanayojengwa na serikali pamoja na taasisi binafsi kwa ajili ya kutoa huduma za kijamii lakini ujenzi huo ,unakuwa kinyume na matarajio kwa watu hawa pamoja na jamii inayotambua haki na usawa kwa binadamu wote,kwani ujenzi huo hauzingatii miundo mbinu au matakwa ya watu wenye ulemavu kutokana na hali waliyokuwanayo ya kimaumbile unakuwa usumbufu kufikia sehemu za juu ndani ya majengo hayo kwani hapana visaidizi vya kisasa vilivyowekwa kwa ajili ya watu hawa.
Unyanyasaji na ubakaji kwa watu hawa jamii inachukulia kama sehemu ya maisha ya watu wenye ulemavu jambo ambalo si busara katika maisha halisi ya wazanzibar nchi yenye sifa za kipekee katika uso wa kidunia kwa wema,heshima,busara ,imani na hekima kwa raia wa nchi hii iliyojaa nyingi amani imetawala kila sehemu ya nchi,lakini hili tujue kuwa ni jukumu la kila mtu kusimamia na kukemea vitendo hivyo viovu ambavyo vinafanyika ndani ya jamii yetu tusitafute nani mchawi juu ya suala hili bali kukae na kutafakali kwa kina jinsi gani kumaliza tatizo hili,vipo vitendo vinavyosikitisha mfano utakuta mtu mwenye ulemavu wa akili anapewa uja uzito na mtu asiyejulikana,kweli katiba ya nchi ambayo ni sheria mama ya nchi inafanya kazi ipasavyo kwa kuwawajibisha watu wanaofanya vitendo vya uzalilisha na ubakaji kwa watu wenye ulemavu kama sheria na kanuni za nchi hazitekelezwi sasa wakati umefika kwa kila mmoja wetu kubadilika kitabia katika kusimamia na kutekeleza mambo yote yanayowahusu watu watu hawa.
Sheria ya watu wenye ulemavu( haki na fursa) na.9 ya mwaka 2006 inasema `watu wenye ulemavu wanatakiwa kuwa na fursa iliyo sawa kwa manufaa ya taifa katika nyanja zote za kijamii na katika elimu,habari,mawasiliano na mazingira ya kimaumbile kama vile lugha ya alama,tafsiri kwa visiwi,kanda,maandishi ya nukta nundu,taarifa na vipindi vinavyotokana na kompyuta,tovuti na kuweka mpangilio wa mazingira halisi kama vile nyumba,majengo,usafiri na mitaa ili waweze kuifikia.
Pia baraza la taifa la zanzibar la watu wenye ulemavu lilianzishwa chini ya kifungucha 26 cha sheria hii kwa lengo la kusimamia haki na maslahi ya watu wenye ulemavu nchini.
Kwa mujibu wa sheria hii kila jamaa wa mtu mwenye ulemavu atakuwa na wajibu wa kutoa haki na fursa kwa mtu mwenye ulemavu atakayeshindwa kufuata masharti ya kifungu (1) cha kifungu hiki atakuwa ametenda kosa,pale itakapothibitika kwa jamaa ana jhatia ya kuacha kwa makusudi kutoa haki na fursa kwa mtu mwenye ulemavu,mahkama inaweza kwa maombi kutoka kwa mtu mwenye ulemavu au baraza kuamuru kwamba haki na fursa zitolewe kwa usawa.
Mkataba wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu unatambua umuhimu wa misingi na miongozo ya sera iliyokuwemo ndani ya mpango wa vitendo wa dunia kuhusu watu wenye ulemavu na kanuni za kutoa fursa sawa katika ushawishi,uendelezaji,utengenezaji na kuthamini sera,mipango na hatua mbalimbali katika ngazi ya kimataifa,kikanda na kitaifa ili kutoa fursa sawa kwa watu wenye ulemavu.
Katika ibara ya 27 kwenye mkataba wa kimataifa unabainisha nchi zilizoridhia mkataba huo zinatambua haki ya watu wenye ulemavu kufanya kazi kwa misingi sawa na wengine hii inajumuisha haki ya kujipatia nafasi ya kumudu maisha kwa kufanya kazi walioichagua au kuibua katika soko la ajira na mazingira ya kazi yawe wazi,shirikishi na yanafikika na watu wenye ulemavu pamoja na kulinda na kukuza upatikanaji wa haki ya kufanya kazi,ikijumuisha wale waliopata ulemavu wakiwa kazini,kwa kuchukua hatua na sheria inayofaa.
Mwanaharakati wa masuala ya watu wenye ulemavu Zanzibar bw.Ali Saleh ameelezea hisia zake juu ya watu wenye ulemavu hapa nchini katika mafunzo ya siku tatu ya waandishi wa habari juu ya kutambua haki na usawa kwa watu hao amesema bado jamii inatakiwa kubadilika kitabia na kufuata kanuni na sheria za nchi ,pamoja na kutambua na kuheshimu haki za binadamu bila ya kuacha nyuma utamaduni halisi wa mzanzibar ,hayo ni mambo muhimu ya kuzingatia kwa kila mmoja wetu ili nchi yetu iwe miongoni mwa nchi zinazojali na kutambua haki na fursa kwa watu wenye ulemavu.
Bi, Zainabu Khamis Mohamed anaishi na ulemavu wa ngozi (albino) amesema suala la ulemavu ni kasoro ndogo za kibinadamu zinazoweza kutokea kwa binadamu yeyote,hivyo jamii iwashirikishe katika masuala mbalimbali nao wanaweza kushiriki katika ujenzi wa taifa kama watu wengine ni muhimu kuondokana na imani potofu kuwa watu hao hawawezi kufanya kazi au kupata elimu vitu ambavyo ni msingi wa maisha ya kila mtu.
Aidha ametoa wito kwa serikali pamoja na taasisi binafsi kushirikiana katika kuwawezesha kiuchumi ili waweze kujiajiri wenyewe kwani kufanya hivyo kutawasaidia katika masuala mbalimbali ya kujikwamu kimaisha na kuondokana na umasikini.
Kama Mwandishi wa makala hii nina machache kwa jamii kweli yapo matukio mengi ya kusikitisha na kutisha wanayofanyiwa watu wenye ulemavu,lakini mbaya zaidi vyombo vyenye dhamana ya sheria vipo kimya wakati sheria na mkataba wa kimataifa ipo lakini wahusika wanaofanya matukio hayo hawawajibishwi,je kama sheria hazitekelezwi jamii zilizochoka na unyanyasaji na uonevu zitakuwa na imani au uzalendo juu ya nchi yao, tubadilikeni kwani suala la ulemavu si la mtu au watu Fulani kila mtu ni mlemavu mtarajiwa kama si leo basi kesho yaweza ukawa mlemavu wahenga walinena “kama ujafa ujaumbika ”methali hii tuitafakali kisha turudi katika misingi ya dini zetu bila ya kuacha nyuma utamaduni na uhalisia wa maisha yetu ya kila siku.
Ushauri wangu kwa serikali sasa naweza kusema kwamba wakati umefika wa serikali kukunjua mbawa zake katika jamii na kusimamia ipasavyo haki ma fursa kwa watu wenye ulemavu ili nao,waweze kuondokana vilio vya muda juu ya ubaguzi,mateso,machungu yaliyopelekea kukata tamaa kwa walio wengi,ni muhimu kufikiria zaidi juu ya uwepo wa watu hawa wenye uwezo mkubwa wa kiutendaji wakiwezeshwa na kupewa mbinu za kujikwamua pia washirikishwe katika mambo mbalimbali ya kitaifa na kijamii.

No comments:

Post a Comment