Friday, November 4, 2011

Balozi Amina Salum Ali akizungumza na Balozi Seif Ali Iddi

Mwakilishi wa Bara la Afrika katika Umoja wa Mataifa Balozi Amina Salim Ali amewataka Watanzania kulitumia vyema soko la Marekani katika kukuza uchumi wa Taifa.
Balozi Amina alitoa nasaha hizo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na Ujumbe wake ulipomtembelea Ofisini kwake Mjini Washington DC Nchini Marekani.
Amesema Marekani kupitia mashirika na makampuni kadhaa ya Nchi hiyo hivi sasa yameelekeza nguvu katika kuwekeza Vitega Uchumi kwenye Mataifa kadhaa Ulimwenguni.
“ Hakikisheni Watanzania mnachangamkia vyema fursa hizo ambazo wenzetu wa Nigeria, Ethiopia na hata Majirani zetu wa Kenya wanazitumia ”.Alisema Balozi Seif.
Balozi Amina ameziasa taasisi zinazosimamia uwekezaji kuwa makini na wawekezaji wanaoonyesha hamu ya kutaka kuwekeza.
Amesema si vyema kwa wawekezaji hao kuhangaishwa wakati wanapotaka kuwekeza vitega uchumi vyao Nchini.
Balozi Amina ameupongeza Ujumbe huo wa Zanzibar unaofanya ziara Nchini Marekani kwa hatua yake ya kuitangaza Zanzibar kwa wawekezaji wa Marekani kufungua milango ya uwekezaji Zanzibar.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar balozi Seif Ali Iddi alimshukuru Balozi Amina kwa kuwa kiungo muhimu cha mawasiliano kati ya Zanzibar na Wawekezaji wa Marekani.
Balozi Seif alisema Mwakilishi huyo wa Bara la Afrika katika Umoja wa Mataifa amechangia kuifanya ziara hiyo kuwa ya mafanikio kwa kiwango kikubwa.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

No comments:

Post a Comment