Tuesday, August 16, 2011

Karafuu Zanzibar

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepongezwa kwa juhudi zake inazochukuwa katika kuhakikisha Zao la Taifa la Karafuu linauzwa katika Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar { ZSTC }. Pongezi hizo zimetolewa na baadhi ya Mabalozi wa wadi ya Kitope wakati wa kikao chao na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika Ofisi ya Jimbo hilo iliyopo Kinduni .

Mabalozi hao wamesema udhibiti mzuri wa zao hilo pamoja na Bei muwafaka umepelekea Wakulima wa zao hilo kuuza Bidhaa hiyo katika Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar { ZSTC }.Wamesema kiwango kikubwa cha ununuzi wa zao hilo katika kipindi kifupi cha msimu huu kinaashiria mkakati madhubuti uliowekwa na Serikali wa udhibiti wa zao hilo kupitia kamati za Ulinzi, Masheha na Wananchi.

“Nimesikia leo katika Vyombo vya Habari huko Pemba kwamba Tani zisizopungua mia moja zimeuzwa ZSTC . Kwa hilo linastahiki kupongezwa ” Amesema mmoja wa Mabalozi hao Bwana Makame Ali Mussa. Akizungumza na Mabalozi hao wa Wadi ya Kitope Balozi Seif Ali Iddi amewasisitiza kuendeleza Umoja wao wakati wote kwa lengo la kufanikisha Malengo waliyojipangia. Balozi Seif amewanasihi Viongozi hao kujitokeza kugombea nafasi tofauti wakati utakapowadia uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi.

Wakati huo huo Balozi Seif Ali Iddi amekabidhi jumla ya Shilingi Milioni Mbili na laki nne kutunisha Mfuko wa Maendeleo wa Jumuiya wa Wastaafu wa Taasisi za Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.Fedha hizo zimetolewa na Baadhi ya waheshimiwa Wawakilishi na Mbunge wa kikwajuni zimekuswanywa chini ya dhamana ya Balozi Seif kufuatia mchango wa papo kwa papo iliyofanywa tarehe 11 juni mwaka huu.

Akizungumza na Wastaafu hao Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif amesema Jumuiya kama hii kujikusanya katika kujitafutia ajira ni jambo la msingi na huleta Heshima kwao. Amesema huo ni mfano mzuri kwa vile hawakujibweteka katika kujitafutia maisha, hivyo ni vyema kwa wastaafu wa Taasisi za Serikali ya Mainduzi ya Zanzibar kuiga mfano kama huo. Naye mlezi wa Jumuiya hiyo Bibi Tereza Olban Ali amempongeza Balozi Seif kwa jukumu alilolikubali ambalo limeleta faraja kwao.

Waheshimiwa waliochangia mchango huo ni Mwenyewe Balozi Seif Shilingi Milioni 1,000,000/- ,Mwakilishi wa jimbo la Rahaleo Mh. Nassor Jazira Shilingi laki 700,000/- na Mwakilishi wa jimbo la Amani Mh. Fatma Mbarouk Shilingi laki 350,000/- Wengine ni Naibu Waziri wa Habari Mh. Hindi Hamad Shilingi laki 150,000/-, Mwakilishi wa jimbo la Kikwajuni Mh. Mahmoud Mohd Shilingi 100,000/- na Mbunge wa Jimbo la Kikwajuini Mh. Masauni Yussuf Masauni Shilingi 100,000/-.

No comments:

Post a Comment