Tuesday, September 13, 2011

Mola awape Subra wafiwa wote katika kipindi hiki kigumu cha Msiba!


Na Ramadhan Himid, Zanzibar
Mengi yamesemwa na yanaendelea kusemwa juu ya msiba mkubwa uliolikumba taifa huko Zanzibar katika usiku wa kuamkia tarehe 10 Septemba mwaka huu wakati Meli ya MV Spice Islander iliyokuwa ikitokea Zanzibar kuelekea Wete Pemba kuzama katika mkondo wa Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Wale wenye imani inayofanana na mimi huwa kila tunapopatwa na jambo zito kama hili hulielekeza moja kwa moja kwa Mola wetu kwa kusema “Inalillah Waina iraih rajiuun”, yaani, “Sisi sote ni Waja wa Mungu na kwake yeye tu ndio Marejeo”.
Bila shaka lililoandikwa na Mungu halipanguki, na tukiamini hilo tutakubaliana pia kwamba sisi tuliwapenda sana jamaa zetu ila Mungu amewapenda zaidi, na yeye tu pekee ndiye mwenye maamuzi sahihi ya kufanya apendavyo.
Sina lengo la kukumbusha kilio matangani, lakini msiba huu ni mkubwa na umemgusa kila mmoja wetu kwa namna moja ama nyengine na ndio maana tunasema ni msiba wa kitaifa ambapo nami kupitia kalamu yangu hii sinabudi kutoa rambi rambi yangu kwa ndugu zetu tuliowapoteza
Kwa hakika Zanzibar nzima ilijinamia na haikuwa rahisi mtu kujizuia hisia zake na watu walikuwa na kila sababu ya kuangua vilio vyao na hata kushindwa kula.Tunasema ni msiba mkubwa haujawahi kutokea , na tumuombe Mungu atuepushe kwa hili na jengine.Amin.
Mungu atupe subra katika kipindi hiki kigumu kwa kuwapoteza jamaa zetu 197 ambao walifariki dunia na 619 waliookolewa. Ni kipindi kigumu lakini kwa kuwa mwanadamu amepewa sahau, inshaallah Mungu atatupa lenye kheir na sisi zaidi ya hao tuliowapoteza.
Ajali hii mbali na kutukumbusha ajali ya Mv Bukoba iliyotokea Tanzania Bara, bali pia inatukumbusha kuwa ni takribani miaka miwili hivi ambapo MV Fatih ilizama chini ya Bandari Zanzibar May 27, 2009 ambapo tuliwapoteza watu saba.
Mbaya zaidi kinacholeta taharuki kwa ajali hii ya MV Spice Islander ni kwamba idadi halisi haijulikani hadi sasa kwani inasemekana meli hiyo ilisheheni pomoni kuliko uwezo wake wa kawaida huku ikiwa na tani nyingi za mizigo.
Idadi ya waliokata tiketi inasemekana ni 610 lakini hofu ni kwamba majeruhi waliopatikana ni 619 na waliopatikana wamefariki ni 197, ni sawa na 816. Lakini ukifuatilia kwa karibu watu wengi bado wanaendelea kuwatafuta jamaa zao ambao walikuwemo katika meli hiyo, tena wengine wakiwa na watu watano ama zaidi, hebu na tujiulize meli hiyo ilikuwa na abiria wangapi?
Hili ni swali zito ambalo kila mmoja wetu anaweza kuwa na jawabu yake mwenyewe, lakini ni vyema wenye vyombo vya usafiri wa majini pamoja na Mamlaka husika kila mmoja akatekeleza wajibu wake kwa kuweka mbele maslahi ya umma kuliko maslahi yao binafsi. Umefika wakati kuhakikisha kwamba kunakuwepo kwa usimamizi wa karibu wa kuhakikisha kila meli inakuwa na idadi maalum ya abiria na inapakia kadri ya uwezo wake, tuache tabia ya kujali kitu kuliko utu.
Ni vyema pia zikawapo kumbukumbu maalum za wasafiri jambo hili litasaidia sana kujua idadi halisi kuliko kuzusha taharuki mitaani kama ilivyo hivi sasa ambapo kila mmoja anasema vyake.Jambo hili si gumu iwapo kila mmoja atatekeleza wajibu wake ipasavyo kwa kujali uzalendo na uchungu wa nchi yake. Aidha umefika wakati kwa Mamlaka husika kutoa taaluma ya wajibu wa msafiri na haki zake akiwa safarini pamoja na wajibu wa mwenye chombo na wafanyakazi wake aliowaajiri wakiwa wao ndio hasa dhamana wa chombo hivyo wakati wa safari.
Ninalisema hili kwasababu maalum, kwanza inasemekana kuwa chombo hicho kilijaza kupita kiasi na kabla ya kuondoka bandarini hapo kilikuwa tayari kimeshalemewa upande mmoja na hadi baadhi ya waliokata tiketi kuahirisha kusafiri kwa siku hiyo, lakini kwanini wafanyakazi wa chombo hicho nao wakashindwa kutimiza wajibu wao kwa kupunguza ama mizigo au abiria badala tu ya kuruhusu kuondoka bandarini ilhali wanajuwa kuwa lolote linaweza kutokea.
Kwa upande wa abiria, naamini walijua kuwa chombo kilijaza kadri ya uwezo wao lakini nao kama binadamu huwa hawapewi haki zao kama wasafiri na hii pia inatokea hata kwa usafiri wa nchi kavu abiri wanapodai kuwa chombo kinaenda mbio hutishiwa kuteremshwa njiani ama ndio dereva akakasirika na kuondeza mwendo zaidi.Ndio maana nikasema taaluma hii izidi kutolewa kuelezea haki na wajibu wa msafiri na msafirishaji wakati wa safari.
Tukishindwa kuyafanya haya kwa kuamini tu kuwa mwenye sukani ndiyo mwenye uamuzi wa kufanya atakavyo, tunaweza tukaharibikiwa mno, lakini kama tutakuwa na utaratibu maalum wa kuwajibishana kati ya mwenye chombo kuhakikisha kuwa chombo chake kinakuwa kizima, dereva (kapteni, rubani, baharia) anajali maisha ya aliowapakia na abiria kujua haki zake kutonyamazia kasoro ambazo zinaweza kupoteza uhai wake ….hapo tutakuwa salama!
Waswahili wanasema “ukupigao ndio ukufunzao”,ni wakati mwafaka hivi sasa kuwa na vyombo vya kisasa vya usafiri pamoja na kuokolea pindipo kutatokea maafa makubwa kama haya,Mungu atuepushie.
Serikali yetu nayo lazima iweke kipaumbele cha pekee kwa kuhakikisha kwamba tunakuwa na vyombo vya kisasa vya usafiri wa majini, kwani wengi wetu tunategemea usafiri wa bahari ambao ndio nafuu kuliko usafiri wa anga kwa safari za kwenda Pemba na Dare-es-Salaam , hasa ikizingatiwa kuwa hakuna usafiri mwengine mbadala kutokana na visiwa vyetu kuzungukwa na bahari.
Kwa kweli taifa limepoteza rasilimali muhimu sana kwa uzembe tu wa watu fulani ,inasikitisha na inauma sana kuona watu wengi wamefariki katika ajali hiyo , hasa wakiwemo wanawake na watoto.
Tuiachie Tume ya Usalama wa Taifa fanye kazi yake, lakini haki lazima itendeke na kusiwepo upendeleo kwa kuwafumbia macho baadhi ya watu ambao tukiendelea kuwafumbia macho kuna siku watatufumbua macho huku tumekufa.

No comments:

Post a Comment