Sunday, September 11, 2011

Method Kilaini ndani ya KCP

MKUTANO MKUU WA KAGERA PRESS CLUB (KPC) Septemba 10, 20
PONGEZI
Kwanza ya yote napenda kuwashukuru kwa heshima ya kunialika niwe mgeni rasmi katika mkutano wenu huu mkuu. Waandishi wa habari ni sehemu muhimu katika jamii na mhimili wa nne wa jamii. Hivyo napenda kuwapongeza kwamba mliamua kuunda chombo kinachowaunganisha katika kutimiza majukumu yenu makubwa ya kuunda jumuiya na jamii ya watu kwa kuwapa habari, kuwaelimisha, kuwahamasisha na kuwapa changamoto. Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Kwa watu wa habari ni rahisi kujikuta wanararuana na kuharibiana kazi badala ya kuungana katika kutoa mema kwa watu bila kukwaza ukweli.
UMUHIMU WA WAADISHI WA HABA
1. Waandishi wa habari na vyombo vyao wana uwezo wa kujenga au kuharibu kwa sababu ndio wnaotoa habari za matukio na watu wanawaamini sana. Tajiri mmoja mmiliki wa gazeti alishindwa kumwaminisha mfanyakazi wake juu ya habari Fulani lakini alipoiweka katika gazeti lake mfanyakazi huyo alikuwa wa kwanza kmumwambia kumbe ni kweli kwa sababu ameviona gazetini. Kuposha habari huleta madhara makubwa kwa jamii.
2. Waandishi wa habari wana uwezo wa kuchokoza hata viongozi wa serikali na kuwafanya watimize wajibu wao. Mnakumbuka sakata la magogo ya miti kutoka Rufiji yaliyosafirishwa kwa wingi hata misitu ikaanza kutoweka, vilikuwa vyombo vya habari vilivyopuliza filimbi na hatua zikachululiwa. Huu ni mfano mmoja kati ya matukio mengi.
3. Vyombo vya habari vinatoa mwanya kwa watu kutoa maoni yao na kufanya sauti ya watu hata wale wanyonge isikike. Sauti ya wasio na sauti.
MAADILI YA WAANDISHI WA HABARI
Inafurahisha kuona kwamba KPC ni wanachama hai na wenye uhusiano mzuri na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Baraza hili lina kazi siyo tu ya kutetea uhuru wa habari kufuatana na ibara ya 18 ta katiba ya Tanzania, lakini vile vile kuhakikisha wanahabari wanafuata maadili ya kazi yao. Ili kukuza heshima ya fani yenu hapa Kagera inabidi muwe wanachama hai kwa matendo katika baraza hilo. Uandishi wa habari bila maadili ni sumu kwa jamii. Mifano mikubwa ni jinsi vyombo vya habari vilivyotumiwa Rwanda na Kenya wakati wa machafuko na mauaji.
Jukumu la mwanahabari ni kutoa ukweli hata ule mchungu kwa ajili ya kujenga na kutibu jamii, kuleta uelewano na siyo chuki, mshikamano na siyo utengano, kujenga na siyo kubomoa. Hiyo kazi mtaifanya kama mtasaidiana kufuatana na maadili yanayotolewa na baraza hilo ambalo ni la hiari, huru na lisilo la kiserikali lililoanzishwa mwaka 1997, likiwa na lengo la kujirekebisha lenyewe ili lisitoe mwanya na sababu kwa wengine ikiwemo serikali kuwabana kwa kisingizio cha utovu wa nidhamu. Muwe na uwezo wa kukosoana na kuambizana ukweli.
UHITAJI WA WANAHABARI MKOANI KAGERA
Mkoa wa Kagera una uhitaji wa kupata wanahabari wengi na makini. Kuna watu wengi nje ya mkoa hasa wanakagera amabao wana kui kikubwa kupata habari za Kagera. Hivyo lengo lenu la kuitangaza ni zuri na lenye tija kwa sisi sote. KPC ina kazi kubwa na nzuri ya kuwasaidia na kuwahamasisha wanahabari wa mkoa wa Kagera kutimiza majukumu yao ya:
a. Kutangaza mambo mengi mazuri yanayofanywa Kagera kwa wanakagera na ulimwengu mzima. Ni ninyi mtaweka Kagera kwenye ramani ili mtu asiulize Kagera ni nini? Mnategemewa kuienzi na kuiuza Kagera, utajiri wa kitalii, mazao yake mazuri, utamaduni wake na mafanikio yake. Ninyi muwe wa kwanza kujifunza na kujua Kagera na utajili wake. Tembeleeni sehemu mbali mbali na kutaneni na watu mbali mbali.
b. Kurahisisha kuomba misaada kwa ajili ya Kagera wakati wa shida na maafa kwa kuyatangaza. Mfano ni kimbunga kilichopiga Muleba. Ilituwia rahisi kuomba misaada nje kwa sababu taarifa ilitoka kwenye vyombo vya habari na hatukupashwa kutoa maelezo mengi. Hivyo juzi nilikwenda huko kugawa mabati na mashuka kutoka Caritas Tanzania kwa niaba ya kanisa Katoliki, ninawashukuru sana.
c. Kusisimua viongozi mara nyingine kutoka usingizini kwa kuyaainisha matatizo ambayo hawajayafanyia kazi. Kazi yenu siyo kila mara kufuatana nyuma ya viongozi na kuripoti majigambo yao na kuwafurahisha, nendeni na kule amabako wamesahau na kuonyesha uozo uliopo. Msiogope, mwandishi wa habari anayeogopa na kuwa kibaraka mradi kula hatakuwa hata siku moja mwandishi makini mwenye kuheshimiwa. Fichueni uozo, uzembe na hata ufisadi kama upo hapa Kagera na hapo vitafanyiwa kazi.
d. KPC iwe shule kwa ajili ya waandishi wadogo ambao bado hawajapata elimu kubwa ya uandishi ili waweze kuleta habari kutoka vijijini. Nashukuru na hongera nma uhusiano mzuri na (MCT) na Mfuko wa Habari Tanzania (TMF) na mmefanya kwa mafaniko mradi mkubwa nao, na wao wako tayari kuendelea nanyi. Hivyo hakikisha wale mtakaowachagua wawe na uwezao wa kuendeleza juhudi hizo.
e. Chama kitoe msaada kwa magazeti na vyombo vya habari vya hapa mkoani Kagera na kuanzisha vingine. Najua wengi kula yao ni magazeti na vyombo vya habari vya jijini Dar es Salaam na Mwanza na sina ugomvi nal kwa sababu na linatusaidia kupeleka habari na maoni yetu taifani. Lakini ujuzi wenu usaidie vile vile vyombo vya matumizi ya ndani ili Bukoba/Kagera iwe kituo cha habari (hub).
f. Vyombo vyetu vya habari viwe uwanja wa wanachi kuleta maoni, mawazo, furaha, manunguniko na mafaniko yao kwa umma. Nafurahi sana kusikiliza redio zetu.
g. Changamoto moja ni kwamba waandishi wa habari wengi wako hapa Bukoba mjini na wilaya nyingine hazina hata mmoja. Nilikuwa Muleba Mkuu wa wilaya akaniambia kule hakuna mwandishi hata mmoja, nikashangaa. Najua ninyi hamtahamia Muleba lakini mnaweza kuwahamasisha wana Muleba walu wachache wakajihusisha na uandishi wa habari hata kama siyo wataalamu wakubwa nanyi mkahariri habari hizo. Vile vile haitoshu ninyi kuandika habari za Dar es salaam tu na labda kidogo za Bukoba mjini hasa wanapotembelea viongozi wa juu bali fanya utafiti juu ya sehemu zote za Kagera.
WANAHABARI KAMA FAMILIA MOJA
Inajulikana kwamba magazeti na vyombo vya habari vina wenyewe na kila mwenye chombo ana lengo lake. Mwandishi au mtangazaji lazima afuate sera ya mwenye chombo na vingine vinapingana katika mielekeo yao. Kwetu hilo siyo baya kwa sababu linatupa sisi wadau mitazamo tofauti ili nasi tuweze pupambanua kati ya pumba na mchele. Licha ya hilo ninyi wanahabari mnapashwa kuwa marafiki na ndugu bila uhasama ingawa mara nyingine mnapingana katika maandishi yenu mradi usiseme uongo bali iwe tu ni mitazamo na mkazo tofauti katika ukweli huo huo.
Mkiwa familia moja hapo mipango yenu ya maendeleo itafanikiwa. Leo uko gazeti/radio/TV ya mlengo wa kulia, kesho utakuwa na lile la mlengo wa kushoto bali wewe ubaki mwanahabari. Pawepo uwezekano wa kuketi na kuchambua pamoja habari ndani na nje ya vyombo vya habari ili kupanua ugo wenu. Kuwa na miradi ya pamoja kama vyombo vya habari, mini press na hata SACCOS ya kujikimu. Mwanahabari mwenye njaa husaliti fani yake kwa sababu hulipwa kupindisha habari ambacho ni mwiko na aibu kwa manahabari na madhara yake ni makubwa kwake binafsi na kwa jamii.
Ni vizuri sana kwamba mnaweka mazingira kwa wale wadogo kufanya kazi kama kuwapa kamera, scanner, computer, printer vya kuandikia stori zao na mengine. Kupitia hapo watajifunza na kukua kuwa wanahabari wanaojitegemea.
Uanachama siyo tu kupata faida lakini vile vile una majukumu yake. Mafanikio hutokana na jasho na juhudi. Ukiwa mwanachama kwa mfano itabidi ulipe ada yako mapema ili chama kimudu kazi zake, ushiriki katika mikutano inapoitwa, uchangie kwa namna mbali mbali kwa hali na mali. Asiyetupa haokoti, tupa kwanza na hapo utaokota mengi. Uwajibike, mkipata mradi wa kutekeleza, usaide kuutekeleza vizuri na kutoa ripoti zote zinazohitajika kwa wakati ili waweze kuwaamini na kuwapa miradi mingine. Usiganganie marupurupu ya miradi bila kuitolea jasho lako. Asiyefanya kazi asile.
UCHAGUZI
Mimi simpigii ye yote kampeni na wala sijui nani anagombea, ila nawaombea uchaguzi wenye tija na uwaweke viongozi waostahili na wenye sifa katika safu za kutoa maamuzi. Wawe viongozi wabunifu wataoimarisha siyo tu vilivyopo bali watabuni na njia nyingine za kukiendeleza chama na fani ya uandishi Kagera kwa ujumla. Wawe viogozi wawajibikaji na waaminifu wataoaminiwa siyo tu nanyi lakini hasa wafadhili wa nje ili misaada inayotolewa ifikie lengo lake kwa wakati na kwa mafanikio. Viongozi wa heshima na ustaarabu ambao wataheshimiwa na wote hata viongozi wa serikali na taasisi nyingine ili wawe na uwezo wa kuwasilana nao bila shida. Viongozi wenye kujali kiasi kwamba wataweza kuwasiaidia vijana wanaotaka kuingia fani hii lakini hawajui waanzie wapi au wameingia lakini bado wanyonge bila kuwadhalilisha, kuwakandamiza au kuwaomba hongo.
Ndugu mwenyekiti napenda kumalizia kwa kuwatakia kila la heri na fanaka katika mkutano wenu mkuu ambao utatoa vingongozi bora wa kusimamia fani hii muhimu katika kipindi kijach cha miaka mitatu hapa Kagera. Sisi tuko pamoja nanyi.
Mwenyezi Mungu awabariki
+Method Kilaini
Askofu Msaidizi
Jimbo Katoliki la Bukoba

No comments:

Post a Comment