Tuesday, July 16, 2013

Dk.Shein atowa salama za rambi rambi kwa mkuu wa majeshi Tz

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, pamoja na wananchi wa Zanzibar wamepata mshtuko na huzuni kubwa kwa vifo vya wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi wa Watanzania walioshambuliwa na kuuawa wakati walipokuwa wakilinda amani katika eneo la Darfur, nchini Sudan.

Dk. Shein ameelezea kusikitishwa kwake na vifo hivyo na kueleza kuwa inasikitisha zaidi kuwa wanajeshi hao wamekufa wakiwa katika kazi ya kulinda amani nchini humo na kueleza kuwa wao ni mashujaa na wamekufa kishujaa.


Hayo yalielezwa katika salamu zake za rambi rambi alizotuma Dk. Shein kwa Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananachi wa Tanzania, Jenerali Davis Adolf Mwamunyange pamoja na wanajeshi wote, pia, salamu hizo zilitoa pole kwa familia za wafiwa.


Aidha, salamu hizo alizozituma Dk. Shein zilieleza kuwa huu ni msiba wa Taifa lote na wananchi wote wa Zanzibar wanaungana pamoja katika kuomboleza msiba huo.


“Tunatoa pole na tunamuomba MwenyeziMungu aziweke pahala pema peponi roho za mashujaa hao, vile vile tunawatakia nafuu ya haraka majeruhi wote wa tukio hilo”.


Alisisitiza Dk. Shein “ Mwenyezi Mungu akupeni moyo wa subira na ustahamilivu katika kipindi hiki cha msiba mkubwa”. zilieleza salamu hizo za rambirambi


Dk. Shein pamoja na wananchi wa Zanzibar wanaungana na Watanzania wenzao kuwaombea wale wote walioumia katika tukio hilo ili waweze kupona kwa haraka na kuendelea na majukumu yao ya ulinzi wa amani.


Vijana saba wa Jeshi la Wananachi wa Tanzania waliuawa baada ya kushambuliwa na waasi wa Sudan na wengine walijeruhiwa.


Wanajeshi hao wa Tanzania waliopoteza maisha yao pamoja na wale walioumia walikuwa ni sehemu ya askari 37 na ofisa mmoja ambao walikuwa wanasindikiza msafara wa waangalizi wa kijeshi katika eneo la Darfur.


Katika suala la ulinzi wa amani katika eneo hilo la Darfur, Wanajeshi kutoka Tanzania wamekuwa wakifanya kazi nzuri ya ulinzi tokea pale Tanzania ilipoanza kuchangia walinzi katika eneo hilo mnamo mwaka 2007, ambapo vijana hao waliouawa ni miongoni mwa vijana waliokwenda nchini humo Februari mwaka huu.


Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

No comments:

Post a Comment