Tuesday, July 16, 2013

Dk.Shein aipongeza UNICEF

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amelipongeza Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia Watoto (UNICEF), kwa juhudi zake za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar.

Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Mwakilishi wa UNICEF nchini Tanzania Dk. Jama Gulaid, aliyefika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kumtambulisha Mama Francesca Moranditi atakayefanya kazi za Shirika hilo katika ofisi ya Zanzibar.


Katika maelezo yake Dk. Shein aliueleza uongozi huo wa UNICEF nchini Tanzaia kuwa Shirika hilo limekuwa na historia kubwa na mashirikiano na Zanzibar kwa muda mrefu.


Alieleza kuwa UNICEF imeweza kushirikiana vyema na Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo pamoja na huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na kuimarisha sekta ya afya, elimu pamoja na kuwasaidia na kuwajengea uwezo akina mama na watoto.


Dk. Shein katika maelezo yake alisema kuwa Shirika hilo limeweza kutoa msaada wake mkubwa kwa kushirikiana na Shirika la Afya duniani (WHO), katika kuimarisha sekta ya fya hapa nchini.


Alisisitiza kuwa Zanzibar imeweza kujiweka katika nafasi nzuri katika kufikia malengo ya Milenia katika sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya afya kwa kuweza kuungwa mkono na washirika wa maendeleo likiwemo shirika hilo la UNICEF.


“ Kwa upande wangu binafsi pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar tunatoa pongezi kwa UNICEF kwa kuendeleza ushirikiano wake kwetu na kuendelea kutuunga mkono kwa muda mrefu”,alisema Dk. Shein.


Aidha, Dk. Shein alisema kuwa kupungua vifo vya akina mama na watoto hapa nchini ni miongoni mwa mafanikio makubwa yaliopatikana na Setrikali ya Mapinduzi Zanzibar.


Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumkaribisha Mama Morandini hapa Zanzibar na kumuhakikishia kuwa mashirikiano makubwa atayapata kutoka kwa viongozi wa Serikali na wananchi wa Zanzibar kutokana na ukarimu wao na utamaduni wao wa kupenda wageni.


Mapema katika mazungumzo yake, Dk. Jama Gulaid alimueleza Dk. Shein kuwa Zanzibar imepata mafanikio makubwa katika kuimarisha sekta zake za maendeleo na kutoa pongezi zake kwa kuendelea kuwaenzi na kuwatunza watoto.


Alisema kuwa mbali na juhudi hizo Zanzibar imeweza kupata mafanikio katika kupunguza vifo vya akina mama na watoto pamoja na kupambana na Malaria hatua ambayo imeipa sifa Zanzibar ndani na nje ya Bara la Afrika.


Dk. Gulaid alieleza kuwa mabadiliko makubwa yameweza kutokea hapa nchini katika kuhakisha watoto wanapata haki zao za msingi pamoja na mahitaji yao muhimu juhudi ambazo zinaendelea kufanywa na Serikali anayoiongoza Dk. Shein.


Kutoka na juhudi hizo Mwakilishi huyo wa UNICEF nchini Tanzania alimuhakikishia Dk. Shein kuwa Shirika hilo litaendelea kutoa ushirikiano wake na kuendelea kuiunga mkono Zanzibar ili iweze kupata mafanikio zaidi.


Sambamba na hayo, Dk. Gulaid alimueleza Dk. Shein kuwa UNICEF itandelea kuwajengea uwezo wafanyakazi wake pamoja na kuziimarisha ofisi zake zote zilizopo hapa nchini Tanzania ili ziweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.


Nae Mama Francesca Morandini alitoa pongezi na shukurani kwa Dk. Shein kutokana na kumkaribisha Zanzibar na kumuahidi kuwa UNICEF inathamini na kutambua juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Shein hasa katika kuwajali watoto.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment