Sunday, July 21, 2013

Dk.Shein afutarisha Pemba


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein jana ameungana na wananchi wa Mkoa wa Kusini Pemba katika futari maalum aliyowaandalia huko Ikulu ndogo ya Chake.

Akitoa shukurani kwa niaba ya Mhe. Rais Alhaj Dk. Shein, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mhe. Juma Kasim Tindwa alitoa shukurani kwa wananchi wote waliokubali mwaliko na kuhudhuria katika futari hiyo waliyoandaliwa na Rais ambayo imeonesha upendo mkubwa kwao.

Katika maelezo yake, Mkuu wa Mkoa huyo aliwasihi Masheikh katika Mkoa huo kuendelea kuhubiri amani na utulivu kwani hiyo ndio ngao pekee ya kujiletea maendeleo endelevu na kuishi katika maisha ya upendo.

Nao wananchi wa Mkoa wa Kusini Pemba wakitoa shukurani zao ambazo kwa niaba zilitolewa na Sheikh Mohammed Khamis na kueleza furaha za wananchi hao kwa kufutari pamoja na kiongozi wao wa nchi.

Katika maelezo yake Sheikh Khamis alitoa pongezi kwa Alhaj Dk. Shein kwa juhudi zake za kuwa karibu na wananchi katika shughuli mbali mbali za kimaendeleo zikiwemo za kidini.

Wananchi hao walieleza kuwa katika uongozi wa Rais Dk. Shein wameweza kuona uongozi wa uadilifu anaoufanya pamoja na kutumia busara kubwa na unyenyekevu katika kuongoza nchi.

“Tumeweza kuona uadilifu wako mkubwa katika kuongoza nchi ikiwa ni pamoja na kushiriki katika shughuli mbali mbali za kidini zikiwemo ufunguzi wa misikiti katika maeneo mbali mbali”,alisema Sheikh Mohammed Suleiman.

Pamoja na hayo, wananchi hao walimtakia uongozi mwema kiongozi huyo na kuiombea nchi iendelee kuwa na amani na utulivu na kuwasisitiza wananchi kuendelea kushirikiana pamoja.

Rajab Mkasaba, Pemba.

No comments:

Post a Comment