Wednesday, June 6, 2012

Zanzibar yafundwa kuogelea

Mabingwa wa Kampuni inayojishughulisha na masuala ya Mafunzo ya upigaji mbizi na Uokozi ya Nchini Uingereza { In Deep Diver Training } na ile ya L&W inakusudia kuendeleza mafunzo ya uzamiaji kwa Vijana wa Taasisi tofauti hapa Zanzibar baadaye Mwezi wa Novemba mwaka huu wa 2012.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hizo Bwana Jim Kellett alieleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Nyumbani kwake Mazizini Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Bwa Jim alisema mafunzo hayo yatawashirikisha Vijana 30 kutoka Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo KMKM, Shirika la Uvuvi wakiwemo pia wawakilishi wa Taasisi za Utalii.
Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya Mafunzo na Huduma za upigaji mbizi alifahamisha kwamba Taasisi yake imeamua kuendesha Mafunzo kama hayo katika Nchi mbali mbali kwa lengo la kuwajengea uwezo Vijana wa kutumia Vipaji vyao katika Biashara ya upigaji mbizi.
Alisema mbali ya fani hiyo kutumiwa katika masuala ya uokozi lakini pia itasaidia kutoa ajira kwa Vijana waliomo ndani ya Sekta ya Utalii.
“ Sekta ya Utalii hivi sasa imechukuwa nafasi kubwa ya ya mapato na ajira Duniani. Sasa kuwapatia mafunzo ya upigaji mbizi vijana wanaojishughulisha na masuala ya Utalii ni kuwajengea uwezo mkubwa wa ajira ya kudumu kwao”. Alisisitiza Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya L&W na ile ya In Deep Diver Taraining.
Bwana Jim ameelezea kufurahishwa kwake na mazingira mazuri aliyoyashuhudia hapa Zanzibar katika nyanja ya uzamiaji.
Aliishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuzipitia Sheria na Kanuni za Uokozi kwa lengo la kuzifanyia marekebisho ili ziende na wakati wa sasa.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliupongeza uongozi wa Kampuni zote mbili chini ya Mkurugenzi wao huyo kwa uamuzi wao wa kutoa Mafunzo ya Wiki mbili kwa Askari 30 wa Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo Zanzibar { KMKM }.
Balozi Seif alisema Mafunzo hayo Maalum ya uzamiaji yataweza kusaidia uokozi na hata Shughuli za Utalii hapa Nchini.
“ Uamuzi wenu wa kutoa Wataalamu wa kuendesha mafunzo hayo hasa kwa askari wetu wa KMKM unastahiki kupongezwa na Wananchi wote”. Alifafanua Balozi Seif Ali Iddi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliueleza uongozi wa Kampuni hizo kwamba Zanzibar inakusudia kufikia kuwa na Kiwango cha Kimataifa katika masuala ya Uzamiaji.
Alifahamisha kwamba Kiwango hicho kinakadiriwa kwenda sambamba na uanzishwaji wa Vituo visivyopunguwa sita vya huduma za Uokozi katika sehemu mbali mbali Unguja na Pemba.
Bwana Jim Kellett na Timu yake alikuwepo Zanzibar kuendesha mafunzo ya Wiki mbili kwa Askari 30 wa Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo Zanzibar {KMKM }.

No comments:

Post a Comment