Friday, June 8, 2012

Msumbiji yakumbusha ufugaji wa samaki Zanzibar

Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa Msumbiji imekumbushwa tena kufikiria ombi la Zanzibar la kuipatiwa Wataalamu katika kuendeleza Sekta ya ufugaji wa Samaki wa Kamba.
Ombi hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati wa mazungumzo yake na Balozi wa Msumbiji Nchini Tanzania Bwana Zakaria Kupela yaliyofanyika hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Msumbiji imekuwa na uzoefu wa muda mrefu katika shughuli za ufugaji wa kamba  na kujipatia umaarufu sehemu mbali mbali Duniani.
Alisema utaalamu na uzoefu ulioipata Nchi hiyo unaweza kuisadia Zanzibar katika moja ya harakati zake za kujenga mazingira ya ajira kwa Vijana wake.
“ Sio mbaya kukukumbusha tena lile wazo letu nililokuelezea  wakati ule tulipokutana kwa mara ya kwanza ingawa inaonekana kulikuwepo na tatizo la ufuatiliaji wa suala hilo”. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza Balozi Mdogo wa Msumbiji Bw. Zakaria Kupela kwa juhudi zake za kuendelea kuunganisha uhusiano uliopo kati ya Msumbiji na Tanzania na Zanzibar kwa Ujumla.
Balozi Seif alifahamisha kwamba uhusiano wa pande hizo mbili ni wa maumbile kutokana na maingiliano ya kidamu yaliyopo kati ya Wananchi wa Tanzania na Msumbiji.
Mapema wa Msumbiji aliyemaliza muda wake hapa Tanzania Bwana Zakaria Kupela alishauri rasilmali zilizopo kwa Mataifa yote mawili ni vyema zikawekewa mikataba kwa faida ya Vizazi vijavyo.
Balozi Kupela alisema Mataifa yote mawili yamebarikiwa kuwa na rasilmali nyingi mfano Maji,Madini, Gesi na Bahari ambazo kama hazikuwekewa utaratibu wa matumizi mazuri zinaweza kuchukuliwa na wajanja.
Alifahamisha kwamba Kizazi kijacho kinaweza kukumbwa  na ushawishi wa Baadhi ya Mataifa au mashirika ya Nje katika matumizi ya rasilmali hizo kinyume na  haki ya Mataifa husika.
Alisisitiza suala la kuendelezwa utaratibu wa kubadilishana Wanafunzi kati ya Tanzania na Msumbiji ambao utasaidia zaidi uhusiano wa pande hizo.
Balozi Kupela ameelezea faraja yake kuona nyanja hiyo imeshaleta matunda kwa vile tayari yapo mabadilishano ya wanafunzi 50 wa mwaka wa pili sasa kati ya Tanzania na Msumbiji.
Alisema mpango huo ukiandaliwa vyema unaweza pia kuratibu mafunzo yatakayowawezesha Vijana wa pande zote mbili hizo kuelewa vyema kizazi kilicholeta ukombozi kwa Mataifa hayo mawili.
Kuhusu suala la Amani Balozi Kupela aliwanasihi Wananchi wa Zanzibar kuendeleza amani waliyonayo ndani ya mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa  ambayo hivi sasa ni darasa kwa mataifa mengine Duniani.
Balozi Kupela alitahadharisha kwamba kitu chochote chenye cheche ya kutenganisha jamii ni hatari kwa faifa ya kizazi kijacho.
Balozi Kupela alifika Ofisini kwa Balozi Seif kuaga rasmi na kurejea Nyumbani Msumbiji baaada ya kumaliza muda wake wa Utumishi hapa Tanzania.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

No comments:

Post a Comment