Friday, November 9, 2012

Dr.Shein ampongeza Obama

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein ametuma salamu za pongezi kufuatia ushindi wa Rais Barack Obama wa Marekani katika Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo uliofanyika hivi karibuni.
 
Katika salamu zake za pongezi kwa kiongozi huyo wa Marekani ambaye amechaguliwa kwa mara nyengine tena na wananchi wa nchi hiyo kwa kipindi cha pili, Rais Dk. Shein alieleza jinsi alivyopokea kwa furaha ushindi huo pamoja na wananchi wote wa Zanzibar.
 
Salamu hizo za pongezi zilieleza kuwa kwa niaba yake binafsi pamoja na wananchi wa Zanzibar anatuma salamu za pongezi kwa Rais Obama kwa ushindi mkubwa alioupata katika uchaguzi uliofanyika hivi karibuni nchini humo.
 
Aidha, salamu hizo zilieleza kuwa  wananchi wa Marekani wameona umuhimu wa kumuunga mkono Rais Obama na kumrejesha tena madarakani kwa lengo la kuliendeleza na kuliongoza taifa hilo kubwa duniani kwa kipindi cha miaka mine ijayo.
 
Pamoja na hayo, salamu hizo zilieleza kuwa wananchi wa Zanzibar wanaungana na rafiki zao wa Marekani katika kusherehekea ushindi huo uliotokana na uchaguzi mkuu wa hivi karibuni wa Marekani ambao umempa ushindi Rais Obama.
 
Dk. Shein alimtakia uongozi mwema Rais Obama na kutoa salamu za pongezi kwa familia ya Rais Obama akiwemo Mkewe Mama Michelle Obama  na watoto wake wote Malia na Sasha Obama  pamoja na wananchi  wa Marekani ambao wameonesha wazi imani na uaminifu mkubwa walionao katika uongozi wa Rais Obama.
 
Sambamba na hayo, salamu hizo zilieleza kuwa  uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Zanzibar na Marekani utazidi kuimarika.
 
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment