Friday, November 9, 2012

Balozi wa India akutana na Dr.Shein Ikulu Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameleza haja kwa Serikali ya India kurejesha utamaduni uliokuwa ukifanya miaka ya nyuma wa kuwaleta madaktari bigwa kwa amu hapa Zanzibar hatua ambayo ilisadia sana kuimarisha sekta ya afya na kutoa huduma kwa jamii wakati huo.

Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Balozi mdogo wa India aliopo Zanzibar Mhe. Pawan Kumar ambaye alifika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha.


Dk. Shein alisema kuwa mnamo miaka ya 1970 hadi mwanzoni mwa miaka ya 1980, India ilikuwa na utaratibu huo wa kutela madaktari bingwa hapa Zanzibar ambao waliweza kufanya kazi zao na kutoa huduma za afya kwa wananchi hatua ambayo ni busara kuanzishwa tena ili kuendeleza kuimarisha sekta ya afya hapa Zanzibar.


Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa kuwepo kwa madaktari bigwa hapa nchini kutoka India kutasaida zaidi kuimarisha huduma katika hospitali za Zanzibar hasa hospitali za Wete na Chake kisiwani Pemba ambazo kwa hivi sasa zina upungufu wa madaktari bigwa.


Mbali na hatua hiyo, Dk. Shein alisisitiza umuhimu wa kubadilishana uzoefu na utaalamu kwa madatari wa India na Zanzibar kwa awamu, juhudi ambazo zitasaidia kuipinguzia gharama Serikali ya kupelekea wagonjwa katika hospitali zilizopo nchini humo.
 
Aidha, Dk. Shein alieleza haja ya kuanzisha Mkataba wa Makubaliano juu ya kuimarisha sekta ya afya kati ya India na Zanzibar.

Pia Dk. Shein alimueleza Balozi huyo uhusiano wa siku nyingi katika sanaa ya uimbaji ambao upo kati ya India na Zanzibar hali ambayo ilimpelekea mwimbaji maarufu marehemu Siti Binti Saad kwenda kurikodi katika studio za nchi hiyo nyimbo zake mbali mbali ambazo zilimjengea sifa kubwa duniani.


Kwa upande wa sekta ya kilimo, Dk. Shein alieleza kuwa kutokana na India na Zanzibar kufanana kijiografia kuna umuhimu wa nchi hizo kuendeleza ushirikiano katika sekta hiyo ambayo ni tegemeo kubwa la uchumi wa Zanzibar na wananchi wenyewe.


Dk. Shein alieleza kuwa India ni miongoni mwa nchi zilizopiga hatua katika kufanya utafiti wa kilimo hivyo alieleza haja ya kuimarisha ushirikiano katika sekta hiyo hasa kwa kushirikiana na wataalamu wa Kitengo cha Utafiti wa Kilimo kiliopo Kizimbani.


Kutokana na Balozi huyo kuwa mpya katika mazingira ya Zanzibar Dk. Shein alimshauri kutembelea katika maeneo ya kilimo cha mpunga ili aweze kuona uhalisia na hatua zilizofikiwa na wananchi pamoja na juhudi za serikali za uimarishaji wa sekta hiyo.


Akieleza juu ya zao la karafuu, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa kwa vile India wana historia ya ununuzi na utumiaji wa karafuu kutoka Zanzibar hivyo ipo haja kya kuimarisha ushirikiano wa kibiashara katika zao hilo.


Pia, Dk. Shein alipongeza maendeleo makubwa yaliofikiwa na India katika sekta ya elimu na kueleza kuwa nchi hiyo hivi sasa imekuwa ikitoa mafunzo mbali mbali kwa wanafunzi kutoka nchi tofauti duniani na kueleza kufarajika kwake kutokana na wanafunzi wengi wanaotoka Zanzibar na kwenda nchini humo kusoma fani mbali mbali.


Sambamba na hayo, Dk. Shein alisisitiza haja ya kuendeleza ushirikiano katika sekta hiyo ya elimu huku akipongeza juhudi za India za kutaka kuanzisha Chuo cha Mafunzo ya Amali huko kisiwani Pemba pamoja na juhudi za kuanzisha mradi wa kutoa mafunzo kwa watoto wa kike vijijini.


Nae Balozi huyo mdogo wa India aliopo hapa Zanzibar Mhe. Pawan Kumar alimueleza Dk. Shein kuwa nchi yake itaendeleza uhusiano na ushirikiano uliopo ambao ni wa muda mrefu na umekuwa na historia kubwa.


Balozi Pawan Kumar alieleza kupokea rai zilizotolewa na Dk. Shein katika kuimarisha sekta ya afya nchini pamoja kuahidi kuzifanyia kazi ipasavyo.


Alieleza kuwa kwa upande wa sekta ya Afya India itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa nafasi za masomo kwa madaktari wazalendo. Aidha, Balozi huyo alieleza kuwa mbali ya nafasi za masomo kwa madaktari wazalendo pia, nchi hiyo itaendelea kutoa nafasi za masomo katika fani nyengine tofauti.
 

Balozi Pawan Kumar pia, alibainisha kuendeleza ushirikiano katika kuimarisha nishati pamoja na juhudi za kujikinga na maafa.

Pamoja na hayo, Balozi huyo alimueleza Dk. Shein azma ya India ya kujenga Chuo cha Amali kisiwani Pemba, hatua ambayo itasaidia katika kuimarisha sekta ya ajira na kutoa utaalamu kwa wananchi.
 

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment