Friday, March 23, 2012

Sheria ya Uvuvi Zanzibar

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kuziangalia upya Sheria za Uvuvi zilizopo Nchini ili kuona uvuvi haramu ambao unaendelea kukithiri katika sehemu tofauti ndani ya Visiwa vya Zanzibar unaangamizwa kabisa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Hifadhi ya Ghuba ya Menai katika Jengo la Ofisi hiyo liliopo Kizimkazi Wilaya ya Kusini.
Balozi Seif alisema katika kudhibiti wimbi hilo la Uvuvi haramu ameziagiza Kamati za Hifadhi ya mali asili za Baharini kuvichoma moto Vifaa vinavyokamatwa kutokana na Uvuvi huo maramu baada ya kuthibitishwa na Taasisi zinazohusika ya Masuala hayo.
Alisema hakuna mvuvi asiyeelewa nyavu haramu katika shughuli za Uvuvi lakini kinachojitokeza ni ile tamaa ya baadhi ya wavuvi hao ambayo ikiachiliwa inaweza kuvijengea mazingira ya hatari ya baadae vizazi vijavyo.
Balozi Seif alizipongeza Kamati za Hifadhi ya Mali asili ya Baharini hasa ile ya Ghuba ya Menai kwa juhudi zao za kulinda mazingira katika wakati mgumu.
Aliwataka kutovunjika moyo katika kujitolea huko na kuwaahidi kwamba Serikali itaendelea kushirikiana nao katika mapambano dhidi ya wavuvi haramu.
Mapema Katibu mtendaji wa Jumuiya ya Hifadhi ya Ghuba ya Menai Bwana Mohd Suleiman alisema wimbi la Uvuvi haramu hivi sasa linaonekana kuongezeka kwa kasi kwa kisingizio cha ukali wa Maisha.
Bwana Mohd ameiomba Serikali kuwa makini na watendaji wa Baadhi ya Taasisi za Serikali ambao hutumia mamlaka yao kuwapa nguvu Wavuvi haramu kuendelea kuchafua mazingira ya Bahari.
Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati hiyo Nd. Zahor Kamal Hassan alitanabaisha kwamba tabia ya baadhi ya wavuvi kuichezea bahari kwa kuendeleza tamaa ya haraka itapelekea kuiponza Jamii yote.
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alitembelea Jumuiya ya Wafugaji nyuki iliyopo Muungoni { ZABA } ambapo Mtaalamu wa Nyuki Bwana Andrea Nolli alisema yapo mafanikio kiasi kutokana na mradi huo kuendeshwa kitaalamu.
Bw. Andrea alimueleza Balozi Seif kwamba juhudi za makusudi zinahitajika katika kulinda misitu kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa asali ambao unaonekana kupungua kutokana na ukatwaji ovyo wa Miti. Katika ziara hiyo ndani ya Wilaya ya Kusini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alibahatika kuitembelea Redio ya Jamii iliyopo Mtegani Makunduchi 91.9 F.M na kuwataka Vijana hao wahakikishe kile wanachokitangaza kinapokelewa vyema na Wananchi.
Baadaye Balozi Seif aliangalia Skuli ya Migomba Kiongoni inayotowa mafunzo kwa wakulima wa Migomba pamoja na Shamba la Mihogo la Mkulima Salum Iddi ambapo alielezea kuridhika kwake na juhudi za wakulima hao katika kuimarisha sekta ya Kilimo kinachozingatia utaalamu wa kisasa.
Balozi Seif ambae pia Ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM aliweka jiwe la msingi la Mskani ya CCM ya Haturudi nyuma iliyopo Muyuni “C”.
Akiwapongeza Vijana hao kwa kuitikia wito wa CCM wa kujenga Ofisi za Matawi na Maskani zenye hadhi ya Chama Balozi Seif aliahidi kuchangia Mabati yote kwa ajili ya uwezekaji wa Maskani hiyo.
“Mkijenga Tawi au Maskani ya Chama cha Mapinduzi lazima ifanane na Chama Chenyewe” Alisisitiza Balozi Seif.
Balozi Seif alisema Chama cha Mapinduzi kinathamini kazi inayoendelea kufanywa na Wanachama wake ndani ya Mskani na Matawi Nchini kote.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

No comments:

Post a Comment