Friday, October 28, 2011

Balozi Seif aenda Marakani

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi anaondoka Nchini leo kwa safari ya Kikazi ya siku kumi Nchini Marekani.
Balozi Seif aliyepata mualiko kutoka kwa shirika la uwekezaji vitega uchumi Afrika la Nchini Marekani anauongoza Ujumbe wa Viongozi Sita wa Kiserikali akiwemo Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi.
Ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif inalenga Zanzibar kujitangaza zaidi Nchini Marekani katika Uwekezaji kwenye maeneo yaliyomo ndani ya Sekta za Utalii, Biashara, Elimu, Kilimo, Afya, Miundo Mbinu pamoja na Mazingira.
Viongozi anaofuatana nao katika Ziara hiyo ni pamoja na Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Fedha ,Uchumi na Mipango ya Maendeleo Mh. Omar Yussuf Mzee, Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mh. Fatma Alhabib Fereji na Naibu Waziri wa Afya Dr. Sira Ubwa Mamboya.
Wengine ni Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni Mh. Salmin Awadh Salmin, Katibu Mkuu Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko Nd. Julian Raphael, Mkurugenzi wa Taasisi ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar { ZIPA } Nd. Salum Khamis Nassor wakiwemo pia baadhi ya Wafanya biashara.
Balozi Seif na Ujumbe wake ataanza Ziara yake kwa kukutana na Uongozi wa Taasisi ya Biashara na Maendeleo { USTDA } pamoja na Mwakilishi wa Taasisi ya Biashara na Vitega Uchumi inayosimamia Sera ya Biashara { USTR }.
Pia atakutana na Uongozi wa Shirika la Uwekezaji Vitega Uchumi { OPIG } linalofadhili Miradi ya Biashara ambapo siku inayofuata atakaguwa Bandari ya kwanza kwa upokeaji kwa wingi Bidhaa kutoka nje ya Maarekani ya Houston kwenye Ghuba ya Mexico pamoja na kukutana na Washirika wa masuala ya Biashara Mjini Houston.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif na Ujumbe wake ataendelea na ziara yake katika Mji wa Florida kwa kukitembelea Chuo Kikuu cha Kilimo na Ufundi cha Florida { FAMU }. Balozi Seif anatarajiwa kuondoka Washington Nchini Marekani Tarehe 6 Novemba 2011 na kurejea nyumbani akiuacha Ujumbe wake kuendelea na ziara ya siku tatu ya kukutana na Viongozi wa Taasisi mbali mbali za Uwekezaji Nchini humo ukiwemo Uongozi wa Benki Mashuhuri Duniani ya Exim Bank.
Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

No comments:

Post a Comment