Wednesday, June 13, 2012

SMZ ipo pamoja na wananchi wake

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katu hawatowasaliti wananchi wa Zanzibar katika kutoa maoni ya uundwaji wa katiba mpya ya Tanzania. 
Amesema viongozi wataheshimu na kutetea maoni ya wananchi wanatakayoyatoa kwenye Tume ya marekebisho ya katiba, na kutoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kutoa  maoni yao wakati utakapofika.
Maalim Seif ametoa kauli hiyo leo huko Eacrotanal Mjini Zanzibar alipokuwa akizindua kongamano linalohusu Muungano na Mchakato wa mabadiliko ya katiba ya Tanzania lililoandaliwa na kituo cha huduma za sheria Zanzibar.
Amesema kila mtanzania atakuwa huru kutoa maoni yake, na kwamba  ni fursa muhimu kwa Wazanzibari kueleza kero zinazowakabili ndani ya Muungano, badala ya kukaa kimya na kusubiri maamuzi yasiyokuwa na mustakbali mzuri na nchi yao.
Makamu wa Kwanza wa Rais amekiri kuwepo kwa kero nyingi za Muungano ambazo zinahitaji kutatuliwa kwa haraka ili kupunguza malalamiko ya wananchi wa pande mbili za Muungano.
Amefafanua kuwa kwa sasa yapo mawazo mengi kuhusu muundo wa Muungano, lakini amesema ni vyema kila nchi kati ya Tanganyika na Zanzibar ikawa na mamlaka yake kamili, kisha uanzishwe Muungano wa mkataba kwa mambo ambayo nchi mbili hizi zitakubaliana.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kituo cha huduma za sheria Zanzibar Profesa Chris Maina Peter amesema ni muhimu kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika kuunda katiba yao, ikizingatiwa kuwa katiba zilizopita hazikuwashirikisha wananchi moja kwa moja.
Nae Mwakilishi wa Shirika la Ford Foundation kanda ya Afrika Mashariki bwana Maurice Makoloo amesema shirika lake ambalo limekuwa likisaidia miradi mbali mbali ikiwemo kukuza demokrasia na kupunguza umaskini, litaendelea kushirikiana na Tanzania katika mchakato wake wa mabadiliko ya katiba ili kutimiza lengo lake la kukuza demokrasia katika nchi za Afrika Mashariki.
  Hassan Hamad (OMKR).

Tuesday, June 12, 2012

Tume ya taifa ya sayanzi yaombwa kuwahsjihisha wasomi

Uongozi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia Tanzania {costech} umeombwa kushajiisha Wasomi hasa Vijana wa Vyuo Vikuu Nchini kupenda kufanya tafiti mbali mbali zitakazojenga Mazingira ya kumuondoa  Mtanzania kwenye matatizo yanayomkabili.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa ombi hilo katika Hafla fupi ya uzinduzi wa Ofisi ya Tume hiyo ilyofanyika hapo Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja.
Balozi Seif alisema Tafiti kama hizo ambazo zitakuwa na uhusiano wa moja kwa moja na Mwananchi  zinaweza kusaidia kupata Maendeleo kwa kasi zaidi katika Kipindi kifupi kijacho.
Alisisitiza kwamba Serikali kwa upande wake iko tayari kwa namna yoyote ile kutumia vyema matokeo ya Tafiti zinazofanywa na Wazomi wazalendo.
Hata hivyo Balozi Seif alieleza kuwa yapo baadhi ya matokeo ya Tafiti hubakia kuwa siri kwa Taifa lakini mengine yanastahiki kutolewa kwa Wananchi ili waelewe kinachoendelea kwenye maisha yao.
Balozi Seif alieleza kwamba wakati umefika kwa Makampuni pamoja na Viwanda vya hapa Nchini kujenga Utamaduni wa kutoa kazi zao za Utafiti kwa Tume hiyo ili ijipatie fedha za kuendesha shughuli zake za utafiti kama Nchi nyengine zilizoendelea.
Alieleza kwamba Tanzania imepania kuleta maendeleo kwa Wananchi wake kutokana na uamuzi wake wa kutenga Jumla ya shilingi za Kitanzania Bilioni Thalathini { 30,000,000,000/-} kwa ajili ya Utafiti na Maendeleo kwenye Bajeti yake ya Mwaka 2010/2012.
Balozi Seif alifahamisha kwamba Maendeleo bila ya Sayansi na Teknolojia  hayapatikani kwani masuala hayo mawili yanakaribiana katika utekelezaji wake.
Akizungumzia Tume ya Taifa ya nguvu za Atomu Balozi Seif  alielezea kufarajika kwake kutokana na mipango m,izuri ya Taasisi hiyo kuhudumia Zanzibar katika masuala ya usimamizi wa matumizi salama  ya Mionzi.
Balozi Seif alisema ushirikiano wa pamoja wa Taasisi hiyo,Wizara ya Afya Zanzibar na Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani katika kuanzisha  mradi wa Matibabu ya Saratani katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja unafaa kuungwa mkono.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameishukuru Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uamuzi wake wa  wa kusogeza karibu na Wananchi shughuli za  Ofisi ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Tume ya Taifa ya  Nguvu za Atomu.
Katika Taarifa yake Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania Profesa Iddi Suleiman Nyangarika Mkilaha alisema Taasisi yake itaendelea kutoa Elimu sahihi ya matumizi ya Mionzi.
Profesa Nyangarika alisema Taaluma hizo kwa sasa itazingatia zaidi katika sekta ya Viwanda pamoja na Vituo vya Afya ambavyo vinatumia Vifaa vyenye mazingira ya Nguvu za Atomiki.
Mkurugenzi huyo wa Tume ya Nguvu za Atomiki alifahamisha kwamba katika kupanua zaidi huduma zake Taasisi hiyo itaendelea kupima Mionzi katika Mimea ili kujua kiwango sahihi cha kulinda Vyakula kwa ajili yamatumizi bora kwa Wanaadamu.
Mapema Waziri wa Mawasiliano,Sayansina Teknolojia wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Makame Mnyaa Mbarawa alisema Wizara hiyo itaendelea kushirikiana na Wataalamu wa ndani na nje ili kuona Tafiti zinazofanywa zinatmika kwa walengwa ambao ni Wananchi.
Alisema Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia na ile ya Nguvu za Atomiki zimeanzishwa zikiwa na wajibu wa kusimamia tafiti na nguvu za Atomiki Nchini kwa kushirikiana na Taasisi za Kanda na zile za Kimataifa.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Mkamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Friday, June 8, 2012

Msumbiji yakumbusha ufugaji wa samaki Zanzibar

Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa Msumbiji imekumbushwa tena kufikiria ombi la Zanzibar la kuipatiwa Wataalamu katika kuendeleza Sekta ya ufugaji wa Samaki wa Kamba.
Ombi hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati wa mazungumzo yake na Balozi wa Msumbiji Nchini Tanzania Bwana Zakaria Kupela yaliyofanyika hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Msumbiji imekuwa na uzoefu wa muda mrefu katika shughuli za ufugaji wa kamba  na kujipatia umaarufu sehemu mbali mbali Duniani.
Alisema utaalamu na uzoefu ulioipata Nchi hiyo unaweza kuisadia Zanzibar katika moja ya harakati zake za kujenga mazingira ya ajira kwa Vijana wake.
“ Sio mbaya kukukumbusha tena lile wazo letu nililokuelezea  wakati ule tulipokutana kwa mara ya kwanza ingawa inaonekana kulikuwepo na tatizo la ufuatiliaji wa suala hilo”. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza Balozi Mdogo wa Msumbiji Bw. Zakaria Kupela kwa juhudi zake za kuendelea kuunganisha uhusiano uliopo kati ya Msumbiji na Tanzania na Zanzibar kwa Ujumla.
Balozi Seif alifahamisha kwamba uhusiano wa pande hizo mbili ni wa maumbile kutokana na maingiliano ya kidamu yaliyopo kati ya Wananchi wa Tanzania na Msumbiji.
Mapema wa Msumbiji aliyemaliza muda wake hapa Tanzania Bwana Zakaria Kupela alishauri rasilmali zilizopo kwa Mataifa yote mawili ni vyema zikawekewa mikataba kwa faida ya Vizazi vijavyo.
Balozi Kupela alisema Mataifa yote mawili yamebarikiwa kuwa na rasilmali nyingi mfano Maji,Madini, Gesi na Bahari ambazo kama hazikuwekewa utaratibu wa matumizi mazuri zinaweza kuchukuliwa na wajanja.
Alifahamisha kwamba Kizazi kijacho kinaweza kukumbwa  na ushawishi wa Baadhi ya Mataifa au mashirika ya Nje katika matumizi ya rasilmali hizo kinyume na  haki ya Mataifa husika.
Alisisitiza suala la kuendelezwa utaratibu wa kubadilishana Wanafunzi kati ya Tanzania na Msumbiji ambao utasaidia zaidi uhusiano wa pande hizo.
Balozi Kupela ameelezea faraja yake kuona nyanja hiyo imeshaleta matunda kwa vile tayari yapo mabadilishano ya wanafunzi 50 wa mwaka wa pili sasa kati ya Tanzania na Msumbiji.
Alisema mpango huo ukiandaliwa vyema unaweza pia kuratibu mafunzo yatakayowawezesha Vijana wa pande zote mbili hizo kuelewa vyema kizazi kilicholeta ukombozi kwa Mataifa hayo mawili.
Kuhusu suala la Amani Balozi Kupela aliwanasihi Wananchi wa Zanzibar kuendeleza amani waliyonayo ndani ya mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa  ambayo hivi sasa ni darasa kwa mataifa mengine Duniani.
Balozi Kupela alitahadharisha kwamba kitu chochote chenye cheche ya kutenganisha jamii ni hatari kwa faifa ya kizazi kijacho.
Balozi Kupela alifika Ofisini kwa Balozi Seif kuaga rasmi na kurejea Nyumbani Msumbiji baaada ya kumaliza muda wake wa Utumishi hapa Tanzania.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Wednesday, June 6, 2012

Mbaraka Juma Ali anatafutwa kwa kosa la wizi


   Mnamo tarehe 20 may 2012 siku ya jumapili ulifanyika wizi wa mali za ofisi ya zanzibar press club na mali za IS-HAKA OMAR RWEYEMAMU kwa mujibu wa polisi zinakadiliwa kuwa na thamani ya TSH.11,600,000 uliofanywa na kijana anayeitwa Mbaraka Juma Ali mkaazi wa zanzibar,wizi huo ulifanyika katika mtaa wa michenzani block no.7 ghorofa ya tatu mali zilizoibiwa ni pamoja na
                                   1.Radio aina ya panasonic
                                   2.kompyuta aina laptop
                                   3.sanduku   la nguo
                                   4.passport ya kusafiria
                                   5.dvd player.
                                   6.cheti cha kuzaliwa

Zanzibar yafundwa kuogelea

Mabingwa wa Kampuni inayojishughulisha na masuala ya Mafunzo ya upigaji mbizi na Uokozi ya Nchini Uingereza { In Deep Diver Training } na ile ya L&W inakusudia kuendeleza mafunzo ya uzamiaji kwa Vijana wa Taasisi tofauti hapa Zanzibar baadaye Mwezi wa Novemba mwaka huu wa 2012.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hizo Bwana Jim Kellett alieleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Nyumbani kwake Mazizini Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Bwa Jim alisema mafunzo hayo yatawashirikisha Vijana 30 kutoka Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo KMKM, Shirika la Uvuvi wakiwemo pia wawakilishi wa Taasisi za Utalii.
Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya Mafunzo na Huduma za upigaji mbizi alifahamisha kwamba Taasisi yake imeamua kuendesha Mafunzo kama hayo katika Nchi mbali mbali kwa lengo la kuwajengea uwezo Vijana wa kutumia Vipaji vyao katika Biashara ya upigaji mbizi.
Alisema mbali ya fani hiyo kutumiwa katika masuala ya uokozi lakini pia itasaidia kutoa ajira kwa Vijana waliomo ndani ya Sekta ya Utalii.
“ Sekta ya Utalii hivi sasa imechukuwa nafasi kubwa ya ya mapato na ajira Duniani. Sasa kuwapatia mafunzo ya upigaji mbizi vijana wanaojishughulisha na masuala ya Utalii ni kuwajengea uwezo mkubwa wa ajira ya kudumu kwao”. Alisisitiza Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya L&W na ile ya In Deep Diver Taraining.
Bwana Jim ameelezea kufurahishwa kwake na mazingira mazuri aliyoyashuhudia hapa Zanzibar katika nyanja ya uzamiaji.
Aliishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuzipitia Sheria na Kanuni za Uokozi kwa lengo la kuzifanyia marekebisho ili ziende na wakati wa sasa.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliupongeza uongozi wa Kampuni zote mbili chini ya Mkurugenzi wao huyo kwa uamuzi wao wa kutoa Mafunzo ya Wiki mbili kwa Askari 30 wa Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo Zanzibar { KMKM }.
Balozi Seif alisema Mafunzo hayo Maalum ya uzamiaji yataweza kusaidia uokozi na hata Shughuli za Utalii hapa Nchini.
“ Uamuzi wenu wa kutoa Wataalamu wa kuendesha mafunzo hayo hasa kwa askari wetu wa KMKM unastahiki kupongezwa na Wananchi wote”. Alifafanua Balozi Seif Ali Iddi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliueleza uongozi wa Kampuni hizo kwamba Zanzibar inakusudia kufikia kuwa na Kiwango cha Kimataifa katika masuala ya Uzamiaji.
Alifahamisha kwamba Kiwango hicho kinakadiriwa kwenda sambamba na uanzishwaji wa Vituo visivyopunguwa sita vya huduma za Uokozi katika sehemu mbali mbali Unguja na Pemba.
Bwana Jim Kellett na Timu yake alikuwepo Zanzibar kuendesha mafunzo ya Wiki mbili kwa Askari 30 wa Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo Zanzibar {KMKM }.